Skip to main content

Baraza la Usalama lalaani kitendo cha viongozi Mali kukamatwa

Walinda amani kutoka ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA wakiwa kwenye kikao cha haki na maridhiano kwenye jimbo la kati la Mopti nchini humo
MINUSMA/Gema Cortes
Walinda amani kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA wakiwa kwenye kikao cha haki na maridhiano kwenye jimbo la kati la Mopti nchini humo

Baraza la Usalama lalaani kitendo cha viongozi Mali kukamatwa

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali kitendo cha kukamatwa kwa Rais wa mpito wa Mali, Waziri Mkuu na maafisa wengine waandamizi wa serikali hiyo tarehe 24 mwezi huu wa Mei, kitendo kilichofanywa na maafisa wa jeshi la serikali ya Mali.

Rais huyo wa mpito Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouan ambao wamekuwa wakiongoza serikali ya mpito tangu mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti mwaka jana, walikamatwa na askari na kupelekwa kwenye kambi ya kijeshi karibu na mji mkuu wa Mali, Bamako.  
Ni kwa mantiki hiyo Baraza la Usalama limetaka waachiliwe huru mara moja na bila masharti yoyote huku wanajeshi walioasi warejee kambini haraka iwezekanavyo.

Wajumbe hao kupitia taarifa yao waliyoitoa leo jioni wamesisitiza kuunga mkono kwao serikali ya kiraia ya mpito nchini Mali na kutoa wito kwa kurejeshwa kwa serikali hiyo itakayoendeleza mchakato wa uchaguzi na utawala wa kikatiba ndani ya ratiba iliyowekwa ya miezi 18.

Wametoa wito kwa wadau wa Mali kupatia kipaumbele suala la kurejesha kuaminiana na kushiriki katika mashauriano na wawe tayari kufanikisha malengo hayo.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema kuweka kinguvu uongozi wa mpito ikiwemo matumizi ya kijeshi hilo halikubaliki.

Hata hivyo wameonesha wasiwasi wao juu ya athari hasi za tukio hilo katika harakati za sasa za kukabiliana na ugaidi, kutekeleza makubaliano ya Amani na Maridhiano nchini Mali sambamba na kuleta utulivu kwenye maeneno ya kati ya Mali.

Wamesisitiza kuunga kwao mkono harakati za Muungano wa Afrika, na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS na kutoa wito wa wadau wote kuhakikisha kuwa serikali ya mpito ya Mali inarejea madarakani.

Wajumbe hao pia wamesema wanaunga mkono ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA katika juhudi zake za kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa azimio namba 2531 la mwaka 2020 lililopitishwa na Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa.

TAGS: MINUSMA, Mali