Skip to main content

Ni muhimu kuongeza idadi ya wanawake walinda amani katika kufikia amani endelevu-Meja Nyaboga

Mshindi wa  tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa mwaka 2020.
UN/UNIC Nairobi
Mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa mwaka 2020.

Ni muhimu kuongeza idadi ya wanawake walinda amani katika kufikia amani endelevu-Meja Nyaboga

Amani na Usalama

Mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa mwaka 2020 Meja Steplyne Nyaboga kutoka Kenya amesema wanawake walinda amani wako na jukumu muhimu katika ulinzi wa amani ni motisha kwa kila mwanamke mlinda amani kwamba ana uwezo wa kutekeleza majukumu yake licha ya mazingira magumu. 

Soundcloud

 

Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Meja Nyaboga amesema, “nadhani tuzo itakuwa motisha kwa sababu itatoa changamoto kwa wanawake wengine kuona kama iwapo mimi niliweza kushinda na niliweza kujishughulisha na ulinzi wa amani ni muhimu nao wakachukue jukumu hilo.” Ameongeza kwamba ni muhimu wanawake wasichukulie kazi ya lulinzi wa amani kama ya wanaume tu. 

Akizungumza kuhusu kilichomchagiza kuingia katika ulinzi wa amani amesema, “kwa kweli niliona wanawake wengine ambao walikuwa wanajihusisha na shughuli za ulinzi wa amani na kuona kwmaba iwapo wanawake hao waliweza nami pia ni kama mwanamke naweza kuchangia katika ulinzi wa amani. Na kwangu naamini mchango wangu mdogo katika kubadilisha maisha ya mwanamke au msichana katika mazingira magumu inaniridhisha na ni motisha katika kutekeleza najukumu ya ulinzi wa amani.” 

Tweet URL

Meja Nyaboga amesema kilichomchochea kuingia katika uanajeshi ni, “wakati nilikuwa ningali nasoma nilikuwa na jirani yangu ambaye alikuwa mwanajeshi na nilipokuwa nikimuona n asare yake na magwaride vile vile vyote vilinivutia kutaka kuingia katika uanajeshi, kando na mwonekano wao pia kazi walizokuwa wanazifanya ilinivutia sana kwamba mtu anajitolea maisha yake kwa ajili ya wengine hiyo ilinipatia motisha ya kujiunga na uanajeshi.” 

Kando na kwamba kazi ya ulinzi wa amani ina manufaa kwa jamii husika lakini walinda amani hususan wanawake wanakuabiliwa na changamoto mbali mbali ambapo Meja Nyaboga amesema, “moja ni kukosa kuungwa mkono na familia na hiyo inakatisha mtu tamaa ya kuendelea kwa sababu mawazo yako yatajikita nyumbani na kuathiri utendaji kazi wako.” Ameongeza kwamba, “iwapo haupatiwi kazi ambazo zinakukutanisha na watu usika katika maeneo ya ulinzi wa amani na hivyo kuelewa changamoto zao na mazingira yao na namna ya kuzitatu basi utendaji wako wa kazi utaathiriwa.” 

Hatimaye mshindi huyo wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi wanachama wachangiaji wa vikosi vya ulinzi wa amani akisema, “ni muhimu tutume vikosi vya walinda amani wanawake katika mazingira yanayowahitaji kwa sababu wako na jukumu kubwa la kuangalia maslahi ya wanawake na wasichana walioko katika mazingira hayo, kwani wasiposhughulikia changamoto zinazokumba kundi hilo hakutakuwepo na amani endelevu”. Aidha ameongeza kwamba, “ninasihi nchi wanachama wapeleke wanawake walinda amani kwa sababu ya faida ambazo tumeshuhudia zitokanazo na uwepo wa wanawake walinda amani ili tujenge dunia ilo na amani kamilifu.”