Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yaliyosababishwa na kujaa kwa maji Ziwa Tanganyika yafurusha watu Burundi, IOM yasaidia

Mtoto akiwa amesimama karibu na pampu ya maji iliyozingirwa na maji ya mafuriko huko Gatumba nchini Burundi.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mtoto akiwa amesimama karibu na pampu ya maji iliyozingirwa na maji ya mafuriko huko Gatumba nchini Burundi.

Mafuriko yaliyosababishwa na kujaa kwa maji Ziwa Tanganyika yafurusha watu Burundi, IOM yasaidia

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa  Mataifa la Uhamiaji, IOM na wadau wake wa masuala ya kibinadamu wamesambaza misaada ya dharura kwa familia za watu ambao wamelazimika kukimbia makwao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na kuongezeka kwa kina cha maji cha Ziwa Tanganyika na mto Rusizi.
 

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo mjini Bujumbura, Burundi imesema, “mafuriko ya hivi karibuni yamesababisha watu wengine kukimbia makazi yao huku mali pia zikiharibika. Mgao wa sasa wa misaada ya dharura ukiratibiwa na Idara Kuu ya Ulinzi wa raia na udhibiti wa majanga, unalenga wale ambao wameathirika zaidi na wako maeneo ya Sobel na Kinyinya II.”

Mamlaka za Burundi zimeathibitisha kuwa familia 5,152 zimeathiriwa na kulazimika kukimbia makazi yao tangu wiki iliyopita na IOM Burundi imesambaza misaada ya vifaa visivyo vyakula kama hatua ya kwanza ya usaidizi wa dharura.

Tarehe 23 mwezi huu wa Mei siku ya Jumamosi, IOM ilifanikisha usafirishaji wa familia 254 kutoka miji ya Gatumba na Rukaramu hadi Sobel ambako tayari familia 383 zimepatiwa hifadhi pamoja na misaada ya blanketi, sabuni, mahema na madumu ya kutekea maji.

“Misaada hiyo imewezeshwa na ofisi ya Muungano wa Ulaya, EU nchini Burundi na serikali ya Ujerumani. IOM itasaidia wale walio hatarini zaidi kutoka Gatumba ambao sasa wanaishi Sobel na Kinyinya II,” imesema taarifa hiyo.

Akizungumzia hali halisi ya usaidizi, Mratibu wa IOM nchini Burundi, Michael Asima amesema, “licha yah atua za dhaura za usaidizi zinazochukuliwa hivi sasa, watu wengi bado hawawezi kupata msaada wa kutosha kutokana na uhaba wa rasilimali. Hatuna akiba ya kutosha kukidhi mahitaji yote ya watu ya dharura. Tunataka kuwe na uwezo wa kuwasaidia zaidi malazi na vitu vingine visivyo vyakula.”

Kwa mujibu wa IOM, jamii ya utoaji wa misaada nayo yenyewe haina rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji yanayoongezeka ambayo yanahitaji kuungwa mkono.

Kina cha maji katika Ziwa Tanganyika na mto Rusizi kilianza kuongezeka tangu mwaka jana na hivi karibuni maji yalizidi kutokana na mvua kubwa na kulazima watu kukimbilia nchi jirani za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.