Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imelaani vikali uporaji wa chakula chake cha msaada Jonglei Sudan Kusini

Mgao wa chakula huko Peri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini  ya miaka mitano. (Picha  5 Februari 2019)
WFP/Gabriela Vivacqua
Mgao wa chakula huko Peri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)

WFP imelaani vikali uporaji wa chakula chake cha msaada Jonglei Sudan Kusini

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, limelaani vikali uporaji wa chakula chake cha msaada na uharibifu wa ghala lake la kuhifadhi misaada ya kibinadamu kwenye eneo la Pobor jimboni Jonglei nchini Sudan Kusini.

Taatrifa iliyotolewa leo na WFP mjini Juba imesema machafuko kati ya vikundi vyenye silaha yaliibuka mwezi Mei, na kuwalazimisha maelfu ya watu kufungasha virago na kuhatarisha uwezo wa mashirika ya kibinadamu kusaidia jamii kwenye maeneo yaliyoathirika na njaa.

Kiwango cha tani 550 za chakula cha kutosha kulisha watu 33,000 wasio na uhakika wa chakula kwa mwezi mmoja, kimeporwa au kuharibiwa huko Gumuruk jimbo la Jonglei katika wiki mbili za kwanza za mwezi Mei wakati wa machafuko ya hivi karibuni limesema shirika hilo.

Na kluongeza kuwa chakula hicho kilijumuisha nafaka, kunde, mafuta ya kupikia na virutubisho vya lishe kwa matibabu na kuzuia utapiamlo kwa watoto na wanawake.

Kwa mujibu wa WFP kuongezeka kwa mashambulizi kati ya vikundi vya wenyeji katika mwezi huu wa mei kuelazimisha kumehama wakazi karibu 9,000 kutoka Gumuruk na Lekuangole kwenda kusaka hifadhi katika mji wa Pibor.

"WFP imekasirishwa na ghasia zisizo na maana na wizi wa msaada wake wa chakula huko Gumuruk, ambapo watu wako katika hatihati ya janga la njaa na wanahitaji kila msaada wanaoweza kupata ili kuishi. Chakula kilichoibiwa kilikusudiwa kupelekwa kwa familia masikini zaidi na zenye njaa zaidi ambazo zimepoteza wapendwa wao, mifugo na mali zingine kwa sababu ya vurugu zisizoelezeka na mafuriko ambayo hayajawahi kushuhudiwa kusomba nyumba zao na ardhi, "amesema Matthew Hollingworth, mwakilishi wa WFP na mkurugenzi wa shirika hilo nchi Kusini Sudan.

Ameongeza kuwa mzozo umeathiri kwa kiasi kikubwa jimbo la Jonglei kwa miaka sasa na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, kupoteza maisha na mali, na kuzidisha hali ya kibinadamu kwa jumla kuwa mbaya zaidi. 

Wakati watu milioni 7.24 kote Sudan Kusini wanauhaba wa chakula, karibu asilimia 50 kati yao wako katika majimbo ya Jonglei, Unity na Upper Nile.

WFP inatoa wito kwa pande na vikundi vyote nchini Sudan Kusini kuheshimu kuwepo kwa wafanyikazi wa kibinadamu na mitambo. 

Shirika hilo pamoja na mashirika mengine ya kibinadamu wanafanya kazi kusaidia kupunguza mateso ya watu wa Sudan Kusini huko Jonglei na kote nchini. Mashambulizi kama haya hufanya kazi yetu kuzidi kuwa ngumu ameongeza mwakilishi wa WFP.

Kiwango na ukubwa wa tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula nchini Sudan Kusini kitaendelea kuongezeka kwani Julai na Agosti ni kilele cha msimu wa muambo, wakati familia zimepoteza mavuno yao mengi na wanategemea sana msaada wa chakula. 

Bila kujali uporaji, WFP itaendelea kutoa msaada wa chakula unaohitajika kwa maelfu ya watu walio katika mazingira magumu katika eneo hilo. 

Mwaka jana, WFP ilifikia watu milioni 5.2 kote nchini na msaada wa chakula na lishe.