Mfanyakazi wa Misaada auawa Sudan Kusini

25 Mei 2021

Mashirika ya kutoa misaada na wadau wa Umoja wa Mataifa, wamelaani vikali kile walichokiita ni mwenendo wa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa misaada, na mashambulizi kwenye matukio mawili yaliyofanywa tarehe 21 Mei mwaka huu nchini Sudan Kusini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa Habari mjini New York Marekani amesema, "kwenye tukio la kwanza Daktari, raia wa Sudan Kusini, aliyekuwa anafanya kazi kwenye Kamati ya Uokoaji ya Kimataifa, IRC, aliuawa kikatili katika kituo cha kutolea huduma za afya kwenye jimbo la Unity."

"Tukio la pili lililo tokea kwenye jimbo hilo hilo, ni la msafara wa wafanyakazi 10 wa kutoa misaada wa kamati ya Uokoaji ya Kimataifa kushambuliwa kwa risasi na mtu mwenye silaha nje kidogo ya Kijiji cha Guol, kwa bahati nzuri hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa."

Matukio haya mawili yamekuja siku 10 baada ya mfanyakazi mwingine ya kutoa msaada kuuwawa huko Budi, Katika jimbo la Equatoria Mashariki tarehe 12 mwezi Mei.

Nchini Sudan Kusini zaidi ya watu Milioni 7.2 sawa na asilimia 60 ya idadi ya wananchi wote wanakabiliwa na njaa kali.

Dujarric ameeleza "wafanyakazi wa misaada waliopo nchini Sudan Kusini, wanahofu sana kutokana na kuongezeka kwa mashambulio, uporaji wa vifaa vya misaada ya kibinadamu, na uharibifu wa miundombinu. Hii inafanyika hususan huko Pibor katika jimbo la Jonglei, ambapo Zaidi ya watu 108,000 wanaishi katika maeneo magumu kufikika na wanakabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa chakula."

Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya misaada wanahitaji Dola bilioni 1.7 kuwasaidia watu milioni 6.6 nchini sudan kwa mwaka. Mpaka sassa asilimia 33 ya fedha hizo zimeshapatikana

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter