Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa maji unaua watoto wengi kuliko hata mabomu- UNICEF

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 akisukuma tololi likiwa na madumu ya maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Darfur nchini Sudan
© UNICEF/Shehzad Noorani
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 akisukuma tololi likiwa na madumu ya maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Darfur nchini Sudan

Ukosefu wa maji unaua watoto wengi kuliko hata mabomu- UNICEF

Amani na Usalama

Ukosefu wa maji safi na salama unaweza kuua watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 mara 20 zaidi kuliko mabomu na risasi katika maeneo ya kivita. 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo, jijini New York Marekani ikiangalia maeneo yenye machafuko ya  Mashariki ya Kati, Afrika, Asia na Ulaya na kuonesha kuwa takribani watu milioni 48 wakiwemo watoto wana uhitaji mkubwa wa huduma ya maji safi na salama pamoja na miundombinu ya maji taka.

Mapigano na mizozo kila uchao katika maeneo ya Mashariki ya Kati, Afrika, Asia na Ulaya yanawaweka watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kwenye hatari mara 20 zaidi ya kufa kutokana na kukosa maji kwa kuwa wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya kuhara. 

Ripoti hiyo inasema watoto walio dhaifu sana wapo katika hatari mara nane  zaidi kufariki dunia kama watakosa maji safi na salama ikilinganishwa na watoto waliozaliwa katika mazingira ambapo maji yanapopatikana vizuri. 

Msemaji wa UNICEF programu za Dharura, Manuel Fontaine amesema “Upatikanaji wa maji safi na salama ni njia ya kuimarisha uhai na haitakiwi kamwe kutumika kama mbinu ya kivita”.  Na kuongeza kuwa “kushambulia vyanzo vya maji ni kushambulia Watoto.” 

Mtoto wa kike akiteka maji kutoka katika lori la kusambaza maji kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani huko kaskazini-magharibi mwa Syria
© UNICEF/Khaled Akacha
Mtoto wa kike akiteka maji kutoka katika lori la kusambaza maji kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani huko kaskazini-magharibi mwa Syria

Manuel ametanabaisha namna watoto wanaweza kupoteza maisha akisema, "usambazaji wa maji ukisimama, magonjwa kama kipindupindu na kuhara yanasambaa kama moto wa nyika  na mara nyingi unakuwa na madhara makubwa.” 

 Halikadhalika, “hospitali zinashindwa kufanya kazi, na ongezeko la utapiamlo na uchafu huongezeka. Watoto na familia zao mara nyingi hulazimika kutoka nje kwenda kutafuta maji na huko hujiweka kwenye hatari Zaidi hususani wasichana ambao wanaweza kudhurika na vilevile kukumbwa na vitendo vya kiudhalilishaji “ 

Ripoti imetolea mfano wa maeneo ambayo vita vimeharibu miundombinu na kuwaacha watu katika balaa kubwa la kusaka maji mathalani Yemen watu milioni 15.4 hawana maji.  

Takwimu zilizotolewa kama mfano ni pamoja na Ukraine watu milioni 3.2, ,  Iraq Watu milioni 1.85, Palestina watu milioni 1.6 na Syria watu Milioni 12.2 wote hao wanahitaji maji safi na miundombinu ya maji safi na maji taka kutokana na vilivokuwepo awali kuharikiwa na wapiganaji. 

Nini Kifanyike kunusuru watoto 

Katika kuhakikisha watoto wanalindwa katika maeneo yenye machafuko na kuhakikishiwa usalama wa maji safi nayakutosha UNICEF imeomba mambo makuu 4 yafanyike ikiwemo pande zote zinazoshiriki mapigano mara moja kuacha kuathiri vyanzo vya maji ili kutimiza jukumu lao la kulinda watoto. 

Pili, nchi wanachama pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaokiuka na kushambulia vyanzo vya maji. 

Tatu, watoa misaada kuwekeza kwenye vyanzo vya maji katika maeneo yenye machafuko kwakuwa ndio njia ya kwanza ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko. 

Na Nne, umma kuunga mkono wito wa kusitishwa watoto kushambuliwa katika maeneo yenye machafuko na kupaza sauti zao kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana.