Waliokufa kwa mlipuko wa volkano Nyiragongo wafikia 32.

Kufuatia mlipuko wa volkano katika mlima Nyiragongo, nchini DRC, UNICEF inasema kuwa mamia ya watoto wamepotezana na familia zao na sasa kazi inafanyika kuwaunganisha.
© UNICEF/Olivia Acland
Kufuatia mlipuko wa volkano katika mlima Nyiragongo, nchini DRC, UNICEF inasema kuwa mamia ya watoto wamepotezana na familia zao na sasa kazi inafanyika kuwaunganisha.

Waliokufa kwa mlipuko wa volkano Nyiragongo wafikia 32.

Msaada wa Kibinadamu

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mlipuko wa volkano katika mlima Nyiragongo jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imeongezeka na kufikia wawtu 32 huku Umoja wa Mataifa ukiongeza jitihada za kufikisha misaada. 

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR huko mjini Geneva, Uswisi, Boris Cheshirkov amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa mamlaka za DRC zimetangaza idadi ya waliokufa kufikia 32, ambapo kati yao hao 7 walikufa kwa kufukiwa na lava ya mlima huku watano wakikosa hewa kutokana na kukosa hewa.

Kwa sasa shirika la msalaba mwekundu linaongoza harakati za kuunganisha mamia ya watoto waliotenganishwa na familia zao wakati wakikikimbia mlipuko huo wa Volkano wa tarehe 22 mwezi huu wa Mei.

UNHCR kwa upande wake inatathmini mahitaji ya jamii zilizoathiriwa huko Goma, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Bwana Cherishkov amesema lava hiyo imeunguza nyumba na kulazimu watu wengi kusaka hifadhi kwa majirani na maelfu kadhaa kuvuka mpaka na kuingia nchini Rwanda.

Ingawa lava ilikoma kutoka mlima Nyiragongo siku ya Jumapili, bado kumekuwepo na matetekemo ya ardhi na ziwa la Lava kwenye kreta yam lima inaonekana kujaa tena na hivyo kujenga hofu kuwa kingo mpya zitafunguka na milipuko mipya kuanza tena.

Kwa sasa barabara ya kuelekea jimbo la Kivu Kaskazini imeharibiwa na Lava na hivyo kukwamisha usafirishaji wa chakula kuelekea mji wa Beni na ambako kuna wakimbizi 280,000 waliofurushwa kutokana na mapigano nchini DRC tangu mwezi Januari mwaka huu.

UNHCR itahitaji fedha kusaidia walioathirika wakati huu ambapo ombi la kusaidia DRC la dola milioni 204.8 limefadhiliwa kwa asilimia 17 pekee.