Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani wa Kenya ashinda tuzo ya UN ya Mwaka 2020 ya mwanaharakati wa masuala ya jinsia 

Mlindaamani kutoka Kenya, Steplyne Nyaboga amechaguliwa kupokea tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2020 ya mwanajeshi mwanaharakati wa mwaka wa masuala ya kijinsia
UNAMID
Mlindaamani kutoka Kenya, Steplyne Nyaboga amechaguliwa kupokea tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2020 ya mwanajeshi mwanaharakati wa mwaka wa masuala ya kijinsia

Mlinda amani wa Kenya ashinda tuzo ya UN ya Mwaka 2020 ya mwanaharakati wa masuala ya jinsia 

Amani na Usalama

Mlinda amani kutoka nchini Kenya ambaye hivi karibuni amehitimisha jukumu lake mjini Darfur, Sudan amechaguliwa kupokea tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa mwaka 2020. 

Mshauri wa kijeshi wa masuala ya kijinsia Steplyne Nyaboga, mwenye umri wa miaka 32, ambaye alihudumu katika operesheni ya Umoja wa Mataifa ya mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur (UNAMID) iliyomazikika hivi karibuni, atapokea tuzo hiyo wakati wa hafla itakayofanyika kwa njia ya mtandao ambayo itaongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa Alhamisi, 27 Mei 2021. 

Tuzo hiyo ya “Mwanaharakati wa kijeshi wa mwaka wa masuala ya kijinsia” iliyoundwa mwaka 2016, inatambua kujitolea na juhudi za mlinda amani mmoja wa kijeshi katika kukuza kanuni za Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325 linalohusu Wanawake, Amani na Usalama katika muktadha wa operesheni za amani, kama alivyoteuliwa na wakuu na makamanda wa vikosi vya operesheni za amani za Umoja wa Mataifa. 

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Meja Nyaboga ameonyesha furaha kwamba kazi yake katika upande wa usawa wa kijinsia imetambulika. 

Mlindaamani kutoka Kenya, Steplyne Nyaboga akiendesha mafunzo ya usawa wa kijinsia kwa walinda amani wa kikosi cha Pakistan jimboni Darfur (Kutoka Maktaba)
UNAMID
Mlindaamani kutoka Kenya, Steplyne Nyaboga akiendesha mafunzo ya usawa wa kijinsia kwa walinda amani wa kikosi cha Pakistan jimboni Darfur (Kutoka Maktaba)

Akitanabaisha juu ya jukumu lake kama mlinda amani, anasema: "Nimefurahi sana kwamba juhudi zetu za pamoja katika kutumikia ubinadamu hazikuwa kazi bure. Ulinzi wa amani ni jukumu la kibinadamu, kuwaweka wanawake na wasichana katika kitovu cha juhudi na hofu zetu kutatusaidia kuwalinda vyema raia na kujenga amani endelevu zaidi”.

Meja Nyaboga alipelekwa kwenye ujumbe wa UNAMID mwezi Februari 2019. Katika kipindi chote cha miaka miwili akiwa huko Zalingei, alifanya kazi kwa bidii kutanabaisha suala ya usawa wa kijinsia katika vikosi vya kijeshi kwa kuleta mwamko wa mienendo ya kijinsia mashinani. 

Meja Nyaboga alihimiza ufikishaji wa elimu nyeti ya kijinsia kwa jamii za wenyeji, katika juhudi za kuimarisha ulinzi wa raia. 

Alizingatia pia utoaji wa mafunzo ya kijinsia kwa walindaamani wenzake wanajeshi, na kufundisha karibu asilimia 95 ya kikosi cha jeshi la UNAMID hadi kufikia mwezi Desemba 2020. 

Alishauri pia Kikosi cha jeshi hilo kuhusu jinsi gani ya kutambua na kujumuisha mahitaji ya vikundi vya wanaume, wanawake, wavulana na wasichana katika mazingira hatarishi kwenye uchambuzi, mipango na shughuli za UNAMID, hatua ambayo iliboresha sana uelewa wa kikosi hicho na kushughulikia mahitaji ya ulinzi. 

Akifanya kazi pamoja na wenzake wa masuala ya haki za binadamu, jinsia na mawasiliano, Steplyne pia aliandaa kampeni na warsha kwa wafanyikazi na wanaharakati wa asasi za kiraia kushughulikia maswala yanayoathiri wanawake na wasichana wa Darfur. 

Katibu Mkuu António Guterres amempongeza Meja Nyaboga kwa tuzo yake na kusema"Amani na usalama vinaweza kupatikana na kudumishwa ikiwa wanajamii wote wana fursa sawa, ulinzi, ufikiaji wa rasilimali na huduma na wanaweza kushiriki katika kufanya maamuzi. Kupitia juhudi zake, Meja Nyaboga alianzisha mitazamo mipya na kuongeza ufahamu wa suala muhimu la kijinsia katika Ujumbe wote na kusaidia kuimarisha ushirika wetu na wanawake wa Darfuri. Umoja wa Mataifa unabaki thabiti katika kujitolea kwake kuhakikisha kuwa wanawake wanaketi kwenye meza ya kisiasa na kuweza kuchangia kikamilifu katika amani, na kujitolea kwa Meja Nyaboga kumeendeleza jukumu hili muhimu."

Hii ni mara ya kwanza kwa mlinda amani wa Kenya kupokea tuzo hii ya heshima kubwa.