Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumeafikiana na Iran kuhusu kuendelea ukaguzi na ufuatiliaji wa nyuklia:IAEA 

Rafael Mariano Gross, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA akizungumza na waandishi wa habari mnamo Juni 15, 2020.
IEA/Dean Calmaa
Rafael Mariano Gross, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA akizungumza na waandishi wa habari mnamo Juni 15, 2020.

Tumeafikiana na Iran kuhusu kuendelea ukaguzi na ufuatiliaji wa nyuklia:IAEA 

Masuala ya UM

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA Rafael Mariano Grossi amesema ameafikiana na Iran kuongeza mwezi mmoja zaidi ukaguzi na ufuatiliaji muhimu wa shughuli za nyuklia zinazofanywa na shirika hilo nchini Iran. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Vienna Austria Bwana. Grossi amesema maafikiano hayo yamefikiwa baina yake na Ali Akbar Sahehi, ambaye ni makamu wa Rais na mkuu wa shirika la nguvu za atomiki nchini Iran. 

Chini ya makubaliano yao, taarifa  zilizokusanywa na wakala wa shirika la ufuatiliaji wa vifaa vilivyoorodheshwa katika mkataba wa maelewano ya kiufundi uliosainiwa mwezi wa Februari zitaendelea kuhifadhiwa kwa kipindi kingine cha mwezi mmoja hadi tarehe 24 Juni.  

Pia wamekubaliana pia kuwa vifaa vitaendelea kufanya kazi na kuweza kukusanya na kuhifadhi takwimu zaidi kwa kipindi hiki. 

"Nina furaha kwamba, kupitia mazungumzo yetu endelevu, tumeweza kukubaliana juu ya jambo hili leo. Ninakaribisha maendeleo haya kwani kumalizika kwa muda wa makubaliano ya kiufundi, ambao uliwezesha ukaguzi na ufuatiliaji wa shirika, kungekuwa ni hasara kubwa wakati huu muhimu, " amesema Mkurugenzi Mkuu Grossi na kuongeza kuwa “Makubaliano haya yatahakikisha kuendelea kwa maarifa na upatikanaji wa taarifa japo kwa muda mfupi."