Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la WHO utumike kuimarisha mifumo ya afya- Guterres 

Mhudumu wa afya akijiandaa kumchoma mhudumu mwingine wa afya chanjo ya COVID-19 kwenye hospitali moja huko Mogadishu nchini Somalia.
© UNICEF/Ismail Taxta
Mhudumu wa afya akijiandaa kumchoma mhudumu mwingine wa afya chanjo ya COVID-19 kwenye hospitali moja huko Mogadishu nchini Somalia.

Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la WHO utumike kuimarisha mifumo ya afya- Guterres 

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehutubia mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Shirika la afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni, WHO na kusema iwapo ubaguzi katika utoaji chanjo dhidi ya COVID-19 utaendelea, nchi tajiri zitachanja watu wake wote na kufungua chumi zao huku virusi vikiendelea kusambaa na kubadilika katika nchi maskini na kukwamisha mkwamuko wa uchumi ulimwenguni kote. 

Guterres amesema hali hiyo haitakuwa na faida bali hasara kwa nchi maskini na tajiri kwa sababu “COVID-19 haiwezi kutokomezwa na nchi moja pekee. COVID-10 imeleta tsunami ya machungu. Zaidi ya watu milioni 3.4 wamefariki dunia ulimwenguni kote. Ajira milioni 500 zimetoweka, matrilioni ya dola yamepotea duniani. Walio hatarini zaidi ndio wanaumia na nina hofu hali hii bado haina mwelekeo wa kuisha.” 

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa suluhisho peke ni jitihada zitakazoratibiwa kwa pamoja duniani kote akitaja maeneo matatu ya kuweka uchumi wa dunia katika mwelekeo wa kukwamuka na hatimaye kufanikisha ajenda 2030 na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

Ametaja mambo hayo matatu kuw ani mosi; Dunia lazima ichukue hatua kwa kuazimia na kwa mshikamano kutokomeza virusi vya Corona “viongozi wa dunia lazima waongeze hatua za mpango wa kimataifa wa usawa katika kupatikana kwa chanjo dhidi ya COVID-19, vifaa vya kupima sambamba na matibabu,” akiongeza kuwa hilo lifanyike kupitia mkakati wa kimataifa wa COVAX

UNDP inafanya kampeni ya kuelimisha umma kuhusu COVID-19 katika mji mkuu Mogadishu
UNDP Somalia/Ali Adan Abdi
UNDP inafanya kampeni ya kuelimisha umma kuhusu COVID-19 katika mji mkuu Mogadishu

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa hivi sasa kuna vita dhidi ya virusi vya Corona kwa hiyo mbinu zote za kiuchumi zitumike kuongeza uwezo wa silaha dhidi ya virusi hivyo akisema kuwa ametumia mkutano wa G-20 kusihi nchi hizo kuandaa kikosi kazi chenye wajumbe kutoka nchi zilizo na uwezo wa kutengeneza chanjo, WHO, na wadau wote wa kifedha sambamba na kampuni za dawa, “lengo likiwa angalau kuongeza maradufu uwezo wa uzalishaji wa chanjo na kupatia leseni  na teknolojia ya utengenezaji wa chanjo sambamba na kuondoa vikwazo vya hataza na haki miliki kwenye chanjo hizo.” 

Hatua ya pili kwa mujibu wa Guterres ni kuimarisha mifumo ya afya kwa kutekeleza mpango wa huduma wa afya kwa wote, UHC nah atua ya tatu ni kujiandaa vyema na dharura yoyote ya kiafya inayoweza kutokea baadaye. 

“Mifumo bora na thabiti ya afya ni mwanzo tu lakini haitoshelezi. Naunga mkono mapendekezo ya ripoti ya hivi karibuni ya jopo huru la hatua za kujiandaa dhidi ya milipuko. Dunia inahitaji azma ya kisiasa katika kiwango cha juu ili kubadilisha mifumo iliyopo hivi sasa kupitia njia zinazoratibiwa kimataifa, kiserikali na kijamii,” amesema Katibu Mkuu. 

Guterres amesema ni matumaini yake kuwa mkutano huo wa 74 wa Baraza Kuu la WHO utachukua hatua thabiti za kutekeleza hatua hizo alizopendekeza. 

Mkutano huo unaofanyika kwa njia ya mtandao na kauli mbiu ni  “Kumaliza janga la COVID-19, kuzuia janga lijalo: kujenga pamoja dunia yenye afya na usawa” na utamalizika tarehe Mosi mwezi ujao wa Juni.