Nimejifunza kutunza kumbukumbu- Mlinda amani TANZBATT-8

24 Mei 2021

Kuelekea siku ya walinda amani duniani tarehe 29 mwezi huu wa Mei, tunamulika walinda amani vijana waliojitolea maisha yao ugenini ili kulinda wengine wasio na uwezo wa kujilinda katika nchi zao. Hii ni kwa kuzingatia kuwa ujumbe wa mwaka huu ni Kuelekea amani ya kudumu: Matumizi ya nguvu ya vijana kwa ajili ya amani na usalama.  
 

Ujumbe huu unazingatia kuwa leo hii, makumi ya maelfu ya walinda amani vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 29 wamepelekwa katika operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa kote duniani kwa lengo kuu la kusaidia kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani na raia. Sasa Umoja wa Mataifa kupitia maazimio ya Baraza la Usalama namba 22502419 na 2535 unaongeza ushirikiano na vijana ili kusaidia kusongesha amani.

Na ni kwa kuzingatia hilo tunaelekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kumulika vijana wa kitanzania wanaohudumu katika kikosi cha 8, TANZBATT-8 kwenye Brigedi ya kujibu mashambulizi, FIB ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO. Kituo chao ni Beni, jimboni Kivu Kaskazini.

Kutana na vijana wa Tanzania katika kikosi cha MONUSCO cha kujibu mashambulizi FIB 

Joyce Akany Tweve, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.
MONUSCO
Joyce Akany Tweve, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.

Hii leo tunaanza na Joyce Ackany Tweve mwenye umri wa miaka 24. Jukumu lake la ulinzi wa amani nchini DRC akipeperusha bendera ya Tanzania kupitia TANZBATT-8 chini ya Umoja wa Mataifa ni karani.

Joyce anasema “kama karani kile ninachopenda zaidi ni jinis ambavyo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu yao. Nimeweze kujifunza jinsi ya kutunza kumbukumbu, kupanga nyaraka kiutaratibu na majukumu mengine ambayo napangiwa na wasimamizi wangu.”

Alipoulizwa ni jambo gani amejifunza tangu aanze majukumu yake, Joyce anasema “ni utunzaji wa kumbukumbu na kwamba ni jambo muhimu sana kwa mfanyakazi au katika utendaji kazi kwa sababu itasaidia katika ufuatiliaji pindi jambo fulani linatokea.”

Lucas Julius Matiku, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.
MONUSCO
Lucas Julius Matiku, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.

Huyu ni Koplo Lucas Julius Matiku  mwenye umri wa miaka 23. Koplo Matiku jukumu lake kwenye  ulinzi wa amani ni upashaji wa habari au Mwandishi wa Habari. 

“Kama mlinda amani, kazi yangu ni kuhabarisha wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na jamii ya kimataifa kwa ujumla kuhusu kile kinachoendelea hapa DRC na juhudi za MONUSCO za kuleta amani ili raia waendelee na shughuli zao kama kawaida,” anasema Koplo Matiku.

Akaulizwa ni jambo gani ambalo amejifunza tangu kuanza jukumu lake la ulinzi wa amani akiwa mwanahabari, Koplo Matiku anasema, “ni kwamba kupitia vyombo vya habari, amani inaweza kupatikana, lakini iwapo tutatumia vibaya tasnia hii ya upashaji habari, inaweza kusababisha mizozo na watu wanaweza kugawanyika katika makund iya kiabila na hii inaweza kusababisha kuanza kwa vita.”

Fredrick Urassa, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.
MONUSCO
Fredrick Urassa, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.

Kijana mwingine kutoka TANZBATT-8 anayehuudumu MONUSCO ni Private Fredrick Urassa Paul.

Mlinda amani huyo kutoka Tanzana anasema anachopenda zaidi ni “ni jinsi majeshi kutoka nchi mbalimbali yanaunganisha juhudi zao chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa ili kuleta amani DRC. Halikadhalika ninajihisi vizuri ninapoona raia wana furaha na wanaendelea na maisha yao ya kawaida.”

Lakini ni jambo gani amejifunza zaidi? Private Paul anasema “ni pale panapoibuka kutokuelewana kati ya pande mbili kinzani ndani ya nchi, mashauriano ndio msingi wa kumaliza tofauti zao, badala ya kuanza vita au kupigana. Hii ni kwa sababu wale ambao wanaathirika zaidi ni raia wasio na hatia, hususan wanwake, watoto na wazee.”

TAGS: MONUSCO, Siku za UN, Siku ya Walinda amani, DRC, TANZBATT-8, DRC
 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter