Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bi. Pobee kutoka Ghana kuwa Msaidizi wa Guterres masuala ya Afrika 

Martha Pobee, Msaidizi mpya wa Katibu Mkuu wa UN katika masuala ya Afrika. (Picha - Maktaba
UN /Loey Felipe
Martha Pobee, Msaidizi mpya wa Katibu Mkuu wa UN katika masuala ya Afrika. (Picha - Maktaba

Bi. Pobee kutoka Ghana kuwa Msaidizi wa Guterres masuala ya Afrika 

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa - UN, Antonio Guterres amemchagua Martha Ama Akyaa Pobee kutoka nchini Ghana kuwa msaidizi wake wa Afrika, katika idara  masuala ya Siasa, ujenzi wa amani na kulinda amani.  

Taarifa kutoka mjini New York Marekani, kwa msemaji mkuu wa UN, Stephane Dujarric imesema kuwa, Martha Pobee anachukua nafasi iliyoachwa  wazi na Bintou Keita kutoka nchini Guinea ambaye amekabidhiwa jukumu la kuwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN na Mkuu wa  ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO

Taarifa hiyo ya Dujarric imeongeza “Katibu Mkuu Antonio Guterres amemshukuru Bintou Keita kwa utumishi wake uliotukuka akiwa msaidizi wake kwa masuala ya Afrika na mchango wake katika idara ya kujenga amani na masuala ya kisiasa ya Afrika.” 

Msaidizi mpya wa Afrika, Martha Pobee anaanza kazi akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 kwenye masuala ya kimataifa na kidiplomasia ikiwemo kuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Ghana. 

Pobee amewahi kuwa Mwakilishi wa kudumu wa Ghana katika Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020.