Uwekezaji wa mabililioni ya dola dhidi ya COVID-19 utaokoa matrilioni ya dola na maisha- Guterres 

21 Mei 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehutubia mkutano wa masuala ya afya wa viongozi wa kundi la nchi 20 duniani, G20 na kusema kuwa msingi wa kujikwamua vyema kutoka  janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 na kuzuia majanga ya siku za usoni ya kiafya ni kuwepo kwa huduma ya afya kwa wote na mfumo bora wa huduma ya afya ya msingi. 

Guterres amesema mambo hayo mawili ni muhimu ili kufanikisha lengo namba 3 la maelngo ya maendeleo endelevu duniani, SDGs na ajenda nzima ya 2030. 

Katibu Mkuu amesema hayo huku akikumbusha viongozi hao kuwa mwanzoni mwa janga la Corona alionya kuwa hakuna atakayekuwa salama hadi kila mtu yuko salama akisema, “nilikuwa nahofia juu ya uwezekano wa kuwepo kwa aina mbili ya kasi katika kukabili janga hili. Cha kusikitisisha zaidi hofu yangu imethibitika. Ukosefu mkubwa wa uwiano wa kupata chanjo, upimaji, dawa na vifaa vya matibabu ikiwemo oksijeni, vimesababisha nchi maskini zikitaabishwa na virusi.” 

Kuibuka tena kwa maambukizi India na Amerika ya Kusini 

Katibu Mkuu amesema kusuasua huko na kasi mbili za hatua dhidi ya COVID-19 kumetoa fursa kwa virusi kunyumbulika kwingineko na kuibua hatari kubwa zaidi akitoa mfano wa India na nchi za Amerika ya Kusini. 

 “Msimu wa majira ya baridi unavyosogea katika nchi za kusini, nina hofu kubwa kuwa hali mbaya zaidi itatokea.”  amesema Katibu Mkuu akisema kuwa, kupatia chanjo kila mtu duniani kote na kuendelea na mikakati ya afya kwa umma juu ya kujikinga dhidi ya aina zote mpya za mnyumbuliko wa virusi vya Corona ndio jawabu. 

 Amekumbusha kuwa hadi sasa ni asilimia 82 ya chanzo zote za Corona ndio zimekwenda kwa nchi tajiri huku nchi maskini zikiambulia asilimia 0.3. 

Akisisitiza zaidi Guterres amesema "hebu tuwe wazi, tuko katika vita na virusi. na iwapo uko kwenye vita na virusi tunahitaji kushughulikia silaha zetu kwa kutumia kanuni za kiuchumi na bado hatufikia hapo."  

Guterres amemaanisha kwamba mbinu zinapaswa kubadilika na isiwe kufanya mambo kikawaida iwe kwenye kubadilishana teknolojia, chanjo na kadhalika.

Katibu Mkuu Antonio Guterres akishiriki kwa njia ya video mkutano wa G-20 (Maktaba)
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu Antonio Guterres akishiriki kwa njia ya video mkutano wa G-20 (Maktaba)

Azimio la Roma la nchi za G-20 

Guterres amekumbusha kuwa jawabu la kusambaza chanjo duniani kote ni azimio la Roma la G-20 la kuchukua hatua sahihi kwa kila mtu kupata chanjo, “lakini tunahijita mfumo wa ufuatiliaji, ukiungwa mkono na utashi wa kisiasa ili azimio hilo ligeuke kuwa mpango wa chanjo wa kimataifa duniani.” 

Amesisitiza uratibu wa mipango yote ya sasa ya kufanikisha vita dhidi ya COVID-19 ikiwemo “miongoni mwa mipango mliyotangaza leo. Narejelea wito wangu kwa G-20 ili ianzishwe  kikosi kazi cha pamoja cha  nchi zote zenye uwezo wa kuzalisha chanjo, WHO, mpango wa kufanikisha upatikanaji wa haraka wa vifaa vya matibabu ya Corona, ACT-Accelerator, na wadau wa kifedha na kampuni za madawa na wadau wengine.” 

Katibu Mkuu amesema kikosi kazi hicho kinapaswa kushughulikia mgao sawia wa chanjo duniani kwa kutumia mkakati wa COVAX. 

Guterres amesema kwa upande wake yeye yuko tayari kuhamasisha mfumo wa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha jitihada hizo huku akitoa wito kwa nchi za G-20 kuongoza kwa mfano kwa kuchangia ahadi zao za fedha kwa mfumo wa COVAX kwa kuwa “uwekezaji wa mabilioni ya fedha unaweza kuokoa matrilioni ya fedha pamoja na maisha.” 

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter