Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa ripoti ya Takwimu za Afya Ulimwenguni mwaka 2021 na makadirio ya vifo vya ziada vya COVID-19 

Mtoto wa miezi 7 akipimwa utapiamlo katika kituo cha afya cha jimbo la Yobe nchini Nigeria
© WFP/Arete/Damilola Onafuwa
Mtoto wa miezi 7 akipimwa utapiamlo katika kituo cha afya cha jimbo la Yobe nchini Nigeria

WHO yatoa ripoti ya Takwimu za Afya Ulimwenguni mwaka 2021 na makadirio ya vifo vya ziada vya COVID-19 

Afya

Leo, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limetoa tathmini yake ya kila mwaka ya 'hali ya afya duniani' katika ripoti ya Takwimu za Afya Ulimwenguni mwaka 2021.  

Toleo hili la mwaka 2021 linajumuisha makadirio ya awali ya vifo vya kupindukia vya ulimwengu vinavyotokana na COVID-19 katika mwaka 2020 na hali ya mwenendo wa afya ulimwenguni na kikanda kutoka mwaka 2000-2019. Pia inazingatia kutokuwepo kwa usawa wa kiafya na mapungufu ya data ambayo yameongezwa na janga hilo, na wito wa kuwekeza haraka katika mifumo ya taarifa za afya ili kuhakikisha ulimwengu umeandaliwa vizuri na data bora. 

Taarifa ya WHO iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Uswisi inataja ujumbe muhimu ulioko katika ripoti hiyo ya utafiti kuwa ni kwamba:  

Kuanzia tarehe 31 Desemba 2020, makadirio ya awali yanaonesha idadi ya vifo vya ulimwengu vilivyosababishwa na janga la COVID-19 mnamo mwaka 2020 ni takribani milioni 3, inayowakilisha vifo milioni 1.2 juu zaidi ya vifo milioni 1.8 viliyoripotiwa rasmi. 

“Kulingana na makadirio ya vifo vya ziada kwa mwaka 2020, vifo milioni 3.4 hivi sasa vilivyoripotiwa kwa WHO vinaweza kuwa ni hesabu ya chini, na takwimu za kweli zinaweza kuwa angalau mara 2 hadi 3 zaidi.” Imesema WHO. 

Kila nchi inakabiliwa na changamoto kuripoti vifo vya COVID-19, na WHO inashirikiana na wadau wote kuboresha takwimu na kupata hesabu sahihi. Makadirio ya kimataifa na ya kikanda ya vifo vya ziada itafuatiwa na makadirio ya nchi baadaye mwaka huu. 

Janga la COVID-19 linaleta vitisho vikubwa kwa afya ya watu na ustawi ulimwenguni na inazuia maendeleo katika kufikia malengo ya SDGs na malengo "bilioni tatu" ya WHO. Na asilimia 90 ya nchi zinaripoti kuvurugika kwa huduma muhimu za afya na asilimia 3 ya kaya zimetumia zaidi ya asilimia 25 ya bajeti yao katika huduma za afya mnamo mwaka 2015, na kwa msingi huo, “huduma ya afya kwa wote iko katika hatari ya kurudi nyuma.”  

COVID-19 inaathiri sana watu walio katika mazingira magumu, na wale wanaoishi katika mazingira yaliyo na msongamano wa watu wakiwa katika hatari kubwa. Ukosefu wa data kunachangia matokeo yasiyolingana ya kiafya, na ni asilimia 51 tu ya nchi pamoja na data zilizopangwa katika makundi ya kijamii katika ripoti za kitaifa za takwimu. 

Makadirio ya muda wa kuishi duniani imepanda kutoka miaka 66.8 mnamo 2000 hadi miaka 73.3 mnamo mwaka 2019, na katika maisha ya afya kutoka miaka 58.3 hadi miaka 63.7. Mafanikio makubwa yanapatikana katika nchi zenye kipato cha chini hasa kwa sababu ya kupungua kwa kasi kwa vifo vya watoto na magonjwa ya kuambukiza. 

Matumizi ya tumbaku ulimwenguni yamepungua kwa asilimia 33 tangu mwaka 2000, lakini utipwatipwa wa watu wazima unaongezeka na hadi kufikia  robo ya idadi ya watu katika nchi zenye kipato cha juu kuwa na utipwatipwa mnamo mwaka 2016. “Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yalisababisha vifo 7 kati ya 10 ulimwenguni mnamo mwaka 2019.” Inaeleza WHO. 

WHO imeshirikiana na Microsoft na Avanade kuunda Kituo kipya cha kisasa cha Takwimu za Afya Duniani ili kuboresha ufikiaji wa data, kurekebisha michakato ya data na kutoa data ya afya kwa umma.