Mitungi milioni 4 ya oksijeni yahitajika duniani kote kila siku kwa wagonjwa wa COVID-19 

20 Mei 2021

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limeongeza mara nne mahitaji ya kila siku ya hewa ya oksijeni kwa wagonjwa katika nchi za kipato cha chini na kati, amesema Philippe Duneton, Mkurugenzi wa UNITAID, ambalo ni shirika tanzu la shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO likiwa na wajibu wa kufanikisha uwepo wa tiba nafuu duniani. 

Oksijeni ni dawa muhimu na ya msingi katika kukabili COVID-19 na inaweza kupunguza vifo kwa asilimia 40. 

Ndivyo anavyosema Bwana Duneton, Mkuu wa UNITAID akiongeza kuwa hata kabla ya janga la Corona, nchi za kipato cha chini na kati zilikuwa na uhaba wa Oksijeni, na sasa janga la Corona limeongeza mahitaij zaidi. 

Bwana Duneton amesema mahitaji yameongeza kutoka mitungi milioni moja kwa siku hadi mitungi milioni 4 katika miezi ya karibuni, akitaja sababu za  uhaba kuwa ni uzalishaji, usambazaji na utaratibu wa upataji Oksijeni katik anchi hizo na kubwa zaidi ni uwepo wa oksijeni katika mifumo ya afya kwenye nchi hizo. 

Suluhisho anasema “tunahitaji kuwekeza zaidi na kuongeza usaidizi kwa hizo nchi ili ziweze kuandaa mipango yao, lakini pia tupeleke fedha zaidi kwa hizo nchi ili zipatie oksijeni watu wake.” 

Uhaba wa Oksijeni umeongeza shinikizo kubwa katika hospitali na hivyo kusababisha vifo vingi vinavyoweza kuepukika huku familia zikilipa fedha nyingi ili wapendwa wao waweze kupatiwa mitungi ya oksijeni. 

Mwishoni mwa mwezi Februari, UNITAID, WELLCOME na WHO kupitia mfumo wa kuchagiza vifaa vya matibabu vya COVID-19, ACT Accelerator, waliunda kikosi kazi cha kufanikisha uwepo wa Oksijeni duniani. 

Miongoni mwa nchi ambako wagonjwa COVID-19 wameongezeka na hivyo kuongeza mahitaij ya Oksijeni ni pamoja na Pakistan, Sri Lanka, Ufilipino, Papua New Guinea, Bolivia, Misri, Ethiopia na Afrika Kusini. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter