Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika ni muhimu katika kukwamua uchumi wa dunia

Mwanamke akitengeneza barakoa za kuuza wakati huu wa janga la COVID-19 akiwa Johannesburg Afrika Kusini.
IMF Photo/James Oatway
Mwanamke akitengeneza barakoa za kuuza wakati huu wa janga la COVID-19 akiwa Johannesburg Afrika Kusini.

Afrika ni muhimu katika kukwamua uchumi wa dunia

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu amani na usalama barani Afrika likijikita zaidi na jinsi ya kushughulikia mzizi wa mizozo barani humo sambamba na kusongesha mikakati ya kujikwamua kutoka janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19.

Mwanamke aanza maisha mapya katika kambi ya Doholo nchini Chad baada ya kukimbia mapigano nchini CAR.
© UNHCR
Mwanamke aanza maisha mapya katika kambi ya Doholo nchini Chad baada ya kukimbia mapigano nchini CAR.

Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kujikwamua kutoka janga la Corona ni fursa ya kushughulikia mizizi ya mapigano na mizozo barani humo, kwa kupatia kipaumbele mbinu za kuzuia mapigano na kutekeleza ajenda 2030 ya maendeleo endelevu na ajenda 2063 ya Muungano wa Afrika.

"Mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa unafanya kazi barani Afrika kusaidia kufanikisha malengo hayo. Serikali zenyewe za Afrika nazo zimeazimia kwa dhati kukabiliana na Corona na hata zimeunda kikosi kazi cha kutekeleza mpango wa pamoja wa kukabili janga hilo," amesema Katibu Mkuu.

Hata hivyo amesema juhudi za pamoja za Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika za kukabili COVID-19 zinagonjwa mwamba kwa sababu, "usambazaji usio wa kutosheleza wa chanjo dhidi ya Corona unakwamisha harakati za kujikwamua kwenye janga. Hadi leo hii kati ya chanjo bilioni 1.4 zilizokwishapatiwa wakazi wa dunia, ni chanjo milioni 24 tu ndio zimefika Afrika, ikiwa ni chini ya asilimia 2."

Katibu Mkuu amesema mgao sawia na endelevu wa chanjo ndio njia ya haraka ya kujikwamua kutoka kwenye janga la Corona akisema, "hii inahitaji kugawiana chanjo, kuondoa vikwazo vya kusafisha nje ya nchi chanjo hizo, kuharakisha utengenezaji wa chanjo hizo katika kila nchi na mfumo wa kuchagiza upatikanaji wa chanjo, ACT kupitia COVAX kupatiwa ufadhili wa kutosha."

Hata hivyo amepongeza hatua za misamaha ya madeni kwa nchi maskini akisema kwa hatua za muda mrefu ni lazima kuimarisha na kufanyia marekebisho mfumo wa kimataifa wa madeni.

Sambamba na suala la upatikanaji wa chanjo, Katibu Mkuu amegusia hatua ambazo amekuwa akichukua tangu mwaka jana kuhakikisha kuwa mizozo inakoma Afrika ili kuchochea maendeleo na kufanikisha utokomezaji wa COVID-19.

WHO imeanza kusambaza barani Afrika kitendanishi cha kupima kwa haraka virusi vinavyosababisha COVID-19.
WHO/Africa
WHO imeanza kusambaza barani Afrika kitendanishi cha kupima kwa haraka virusi vinavyosababisha COVID-19.

 

"Tangu janga la COVID-19 lianze nimekuwa natoa maonyo juu ya hatari yake hasa kwa jamii zilizo kwenye mizozo. Nimetoa misururu ya matamko ya kisera ikiwemo lile linalohusu madhara ya COVID-19 kwa Afrika. Hili likuwa chimbuko la wito wangu wa sitisho l amapigano duniani ili kutuwezesha kujikita katika adui yetu mkuu: Vurusi. Wito wangu ulipokelewa na serikali na vikundi vilivyojihami, ikiwemo barani Afrika na ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote ule wakati huu tunapondelea kushuhudia ghasia na mizozo ikiibuka upya," amesema Guterres.

Ametaja maeneo kama vile Cabo Delgado nchini Msumbiji na kule Jamuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC , Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na huko Chad.

COVID-19 na kuporomoka uchumi Afrika na athari kwa wanawake na vijana

Ukuaji uchumi barani Afrika umepungua kwa asilimia 3.4 mwaka huu wa 2021, ikilinganishwa na asilimia 6 duniani. Upelekaji wa fedha nyumbani nao umepungua na kiwango cha madeni kinaongezeka.
Kama hiyo haitoshi, baadhi ya serikali zimetumia janga la Corona kama fursa ya kubinya demokrasia na uhuru wa raia.

Kwa vijana nao, COVID-19 imewasababishia kupoteza fursa za elimu, ajira na njia za kujipatia kipato huku wakikumbwa na mashinikizo ya afya ya akili na kuengulia hali inayowaweka hatarini kusafirishwa kiharamu au kuingia kwenye vitendo vya kihalifu. Guterres amesema na wanawake nao fursa zao zimebinywa na wanaweza kuenguliwa zaidi.

UNDP yapaza sauti

Kwa upande wake, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo, UNDP, limetumia mkutano huo kuelezea hatua zake za kusaidia bara la Afrika kujikwamua kutoka janga la Corona na kusongesha maendeleo.

Akihutubia mkutano huo, Kiongozi Mkuu wa UNDP Achim Steiner amesema ingawa idadi ya vifo na wagonjwa Afrika kutokana na COVID-19 si kubwa, bado wale ambao wameathirika wamekumbwa na madhara makubwa kiuchumi na kijamii.

Hivyo amesema "UNDP inashirikiana na serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine kusaidia uandaji na usambazaji wa chanjo chini ya usimamizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO."

UNDP inafanya kampeni ya kuelimisha umma kuhusu COVID-19 katika mji mkuu Mogadishu
UNDP Somalia/Ali Adan Abdi
UNDP inafanya kampeni ya kuelimisha umma kuhusu COVID-19 katika mji mkuu Mogadishu

Amesema UNDP inajikita katika kuimarisha mifumo na usimamizi ili kuhakikisha kuna uwiano, mnepo na uendelevu katika juhudi za utoaji wa chanjo barani Afrika

"Mathalani huko Equatorial Guinea, UNDP inasaidia serikali kuweka mfumo wa kidijitali wa kuimarisha usambazaji wa chanjo na mifumo ya mnyonyoro wa ufikishaji wa huduma hizo. Nchini Chad, Libya na Mali, UNDP inasaidia kuanzisha mifumo ya kiafya kwenye mtandao. Kwa ujumla ni kuimarisha mifumo ya afya ili iwe bora na hatimaye nchi ziweze kukabilana na majanga ya afya."

Hatua nyingine ametaja umuhimu wa shughuli za kiuchumi zisizoharibu mazingira akipendekeza uwekezaji wa dola bilioni 60 ya kusaidia Afrika kujijenga upya kutoka kwenye janga na hivyo kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Bwana Steiner ametaja pia suala la utawala bora kama msingi wa kujenga jamii zenye usawa na maelewano.