Skip to main content

Biashara ya bidhaa yapiga jeki uchumi wa dunia wakati wa COVID-19:UNCTAD

Mizigo ikiwasili nchini Marekani.
UN News/Daniel Dickinson
Mizigo ikiwasili nchini Marekani.

Biashara ya bidhaa yapiga jeki uchumi wa dunia wakati wa COVID-19:UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Biashara ya bidhaa imekuwa chachu kubwa ya uchumi kuanza kuchipuka tena wakati dunia ikiendelea kupambana na janga la corona au COVID-19 ingawa biashara ya huduma imeendelea kusuasua imesema ripoti mpya iliyotolewa na kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo ikielezea hatua  zilizopigwa katika biashara duniani wakati wa kujikwamua na janga la COVID-19, duniani kote biashara imefikia kiwango cha juu katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 ikiongezeka kwa asilimia 10 mwaka baada ya mwaka na kwa asilimia 4 katika robo ya mwaka. 

Ripoti imeongeza kuwa kilichochochea ongezeko hilo ni biashara ya bidhaa tofauti na biashara ya huduma ambayo bado inasuasua kutokana na kuendelea kwa janga la COVID-19. 

UNCTAD inasema inatarajia kuendelea kwa habari njjema hiyo katika robo ya pili ya mwaka huu wa 2021, huku thamani ya biashara ya bidhaa na huduma ikitabiriwa kufikia dola trilioni 6.6 sawa na ongezeko la mwaka kwa mwaka la karibu asilimia 31% ikilinganisha na ongezeko la chini kabisa la mwaka 2020  karibu asilimia 3% ikilinganishwa na viwango vya kabla ya kuzuka kwa janga la COVID-19 mwaka 2019. 

Ingawa ripoti inatabiri ukuaji wa biashara kwa mwaka mzima wa 2021 kuwa karibu asilimia 16% inasema "bado ukuaji huo unategemea sana kupunguza vizuizi na vikwazo vya COVID-19, mwenendo mzuri unaoendelea wa bei za bidhaa, kwa jumla kujizuia na serra binafsi za kujilinda kibiashara, na hali za uungaji mkono kutoka kwa biashara ndopgondogo na mikakati ya kujikwamua."

Pamoja na habari hizo za matumaini ripoti inasema kujikwamua kibiahsra bado kunatofautiana, haswa miongoni mwa nchi zinazoendelea, huku mauzo ya nje kutoka Asia ya Mashariki yakiongezeka haraka sana huku biashara ya Kusini- Kusini ikibaki kuwa chini ya kiwango cha wastani. 

Na miongoni mwa mataifa ya uchumi mkubwa, mauzo ya nje ya China yanaendelea kuonyesha ongezeko kubwa  wakati mauzo ya nje kutoka Urusi bado yanasalia chini ya wastani uliotarajiwa mwaka 2019. 

Kwa sababu COVID-19 imeendelea kuwa mwiba kwa mataifa mengi ripoti inasema serikali zinatarajiwa kutumia sera tofautitofauti kama sehemu ya mipango yao ya kujikwamua na janga hilo.  

“Kwa kuzingatia msuguano unaoendelea wa kidiplomasia kati ya nchi za  uchumi mkubwa na ugumu wa sasa ndani ya mifumo ya biashara ya pande nyingi, kuna hatari kwamba baadhi ya sera hizi zinaweza kuwa vikwazo vya biashara.” 

Imesema ripoti na kuongeza kwamba “juhudi kuelekea kwenye mazingira na mchakato endelevu wa kujikwamua zaidi zinaweza kuathiri mifumo iliyowekwa ya biashara ya ulimwengu. Kwa mfano, sera zinazolenga kukabiliana na uzalishaji wahewa ukaa kupitia marekebisho ya bei kwa uagizaji zinaonekana kuwa na athari kwa mnyororo wa biashara ya kimataifa”