Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata kabla ya wakimbizi wa Rohingya, tulikuwa hoi, UNHCR imetusaidia - Teknaf, Bangladesh

Wakimbizi warohingya wanaowasili nchini Bangladesh wakiwasili Teknaf, eneo la Cox's Bazar.
UNICEF/Brown
Wakimbizi warohingya wanaowasili nchini Bangladesh wakiwasili Teknaf, eneo la Cox's Bazar.

Hata kabla ya wakimbizi wa Rohingya, tulikuwa hoi, UNHCR imetusaidia - Teknaf, Bangladesh

Wahamiaji na Wakimbizi

Soko la mbogamboga lililofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika moja ya wilaya maskini kabisa ambayo inahifadhi wakimbizi 900,000 wa Rohingya nchini Bangladesh, limekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa eneo hilo ambao mara nyingi wanahangaika kupata mahitaji yao ya kila siku hasa wakati huu janga la COVID-19.

Kabla ya kumiminika kwa wakimbizi wa Rohingya mnamo 2017, wilaya ya Cox's Bazar tayari ilikuwa wilaya isiyo na maendeleo nchini Bangladesh. Kuingia kwa wakimbizi zaidi ya 740,000 kumeathiri zaidi maisha ya jamii za wenyeji. Jamii ya eneo hili ndio walikuwa watoa msaada wa kwanza wakati Warohingya walipowasili bila chochote, hata hivyo, kuendelea kuwepo kwa wakimbizi kumeathiri maisha ya watu wengi wa Bangladesh. Janga la COVID-19 lilisababisha ugumu mkubwa wa kiuchumi na athari za uhakika wa chakula kwa watu wa kawaida walio katika mazingira magumu, na kuwaweka wengi katika hatari ya ukosefu wa chakula. 

Programu mpya, kama vile vituo vya ukusanyaji wa mbogamboga kwa ajili ya kuuza, vimehamasisha watu wengi zaidi kujiingiza katika kilimo. 

Mathana Chakma ni mmoja wa wakulima wanaofaidika na kituo cha kuuzia mbogamboga kilichoanzishwa katika eneo lake na UNHCR na mdau wake wa misaada CNRS. Msichana huyu ambaye aliolewa akiwa na umri wa miaka 16 na kisha kuwa mjane na kurejea kuishi na baba yake na wadogo zake wanne, sasa ndiye anaisaidia familia yake kwa uuzaji wa mazao yake, ambayo ni pamoja na bamia, maharagwe, pilipili, kabichi na mbogamboga nyingine za majani. Mathana anasema,  “Jina langu ni Mathana Chakma. Kuna watu watano katika familia yangu: baba yangu, wadogo zangu watatu na dada, na mimi mwenyewe. Tulilazimika kufanya kazi kwa bidii ili kupata riziki, hata kabla ya watu wa Rohingya kuja.” 

Mathana amepata mara tatu au nne kuhusu ufugaji na kuboresha mbinu za kilimo.  Alipokea pia mbegu, mbolea, mbuzi na kuku, na mwaka jana UNHCR ilimpa ruzuku ya pesa ya dharura kama sehemu ya juhudi ya msaada ya COVID-19, ambayo ametumia kupanua idadi ya mifugo wake. 

Subrata Kumar Chakrabarty, ni Afisa wa UNHCR anayehusika na ustawi wa maisha ya watu katika eneo hilo la Wilaya ya Cox’ Bazar anasema,  "Soko limekuwa na athari chanya kwani hawaitaji kulipa gharama ya usafirishaji. Zaidi, wana nguvu ya kujadiliana kuongeza bei ambayo inasaidia uhakika wao wa chakula." 

Msaada wa UNHCR unafikia maelfu katika makazi ya wakimbizi wa Rohingya na jamii za wenyeji zilizoko karibu kwa kuwapatia mafunzo maalum, mbegu za mazao na pembejeo. Katika nyakati za janga la corona, familia zinapokea pesa pia. Misaada hii imemtoa mtu kama Mathana kutoka katika kukata tamaa na kuwa na matumaini. Anaweza kusaidia familia yake na kukuza matamanio yake mwenyewe kwa ajili ya siku zijazo.