Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaomba raia wa Msumbiji wanaokimbia vurugu wapewe hifadhi nchini Tanzania 

Watu wanaokimbia vurugu jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji kuelekea nchi jirani Tanzania.
© UNHCR/Eduardo Burmeister
Watu wanaokimbia vurugu jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji kuelekea nchi jirani Tanzania.

UNHCR yaomba raia wa Msumbiji wanaokimbia vurugu wapewe hifadhi nchini Tanzania 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, limesema lina wasiwasi mkubwa na taarifa zinazoendelea za watu wanaokimbia jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji kurudishwa kwa nguvu baada ya kuvuka kwenda katika nchi jirani ya Tanzania.

Akizungumza na wanahabari hii leo mjini Geneva Uswisi, Msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov amesema UNHCR na wadau wake wamepokea ripoti za kutia wasiwasi pamoja na ushuhuda wa moja kwa moja kwamba maelfu ya watu kadhaa wa Msumbiji wamerudishwa nyuma kutoka Tanzania kuelekea kaskazini mwa Msumbiji tangu mwaka jana hii ikijumuisha ripoti ya zaidi ya raia wa Msumbiji 1,500 waliorudishwa mwezi ulioipita.  

Mwezi uliopita, yaani Aprili 2021 katika mpaka wa Negomano kaskazini mwa Msumbiji, UNHCR na wadau wake wamegundua kuwa watu wengi wa Msumbiji walioko huko walitarajia kupata kimbilio nchini Tanzania baada ya kukimbia mashambulio mabaya kutoka kwa vikundi visivyo vya serikali huko Palma mnamo mwezi Machi. Watu waliiambia UNHCR walisafiri kwa siku katika mto Ruvuma, wakivuka kwa mashua kufika Tanzania, ambako walirudishwa na mamlaka za nchi hiyo jirani. Wengi walikuwa wanawake na watoto wadogo. 

Msemaji huyo wa UNHCR amesema, “UNHCR inastaajabishwa na ripoti kwamba raia wa Msumbiji wamerejeshwa kwa nguvu na wanazuiwa kutafuta hifadhi. Tunatoa wito kwa pande zote kuruhusu raia wanaokimbia vurugu na mizozo, kutafuta ulinzi wa kimataifa, usalama na usaidizi, pamoja na kuheshimu na kushikilia kikamilifu haki ya kuvuka mipaka ya kimataifa kutafuta hifadhi.” 

Akieleza zaidi kuhusu matukio hayo, Bwana Cheshirkov amesema huko Negomano, watu wameiambia UNHCR walikuwa wametenganishwa na wanafamilia wakati wanakimbia kutoka vijiji vyao nchini Msumbiji, ambapo wengine walitenganishwa baada ya kuwasili Tanzania. Wengi waliripoti kuzuiliwa, kusafirishwa kwenda kwenye shule ya eneo hilo, na kuhojiwa na maafisa wa Tanzania. Wale ambao hawakuweza kutoa ushahidi wa utaifa wa Tanzania walirudishwa Msumbiji kupitia njia tofauti ya mpaka kutoka ule uliotumika kuingia nchini humo wakiwemo watu binafsi au familia za mataifa mchanganyiko. 

“Hali ni mbaya sana kwa mama wasio na wenzi, sasa wanaishi Negomano bila msaada wa familia. Hali katika Negomano ni mbaya na mahitaji ni makubwa kwa chakula, maji na usafi wa mazingira, na huduma za afya, lakini msaada mdogo tu wa kibinadamu unafikia eneo la mbali.” Amesema Cheshirkov.