Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyumbani Tigray machafuko, ukimbizi Sudan ukame, UNHCR yachukua hatua

Maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka kutoka Ethiopia kuingia Sudan wakikimbia mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.
© WFP/Leni Kinzli
Maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka kutoka Ethiopia kuingia Sudan wakikimbia mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Nyumbani Tigray machafuko, ukimbizi Sudan ukame, UNHCR yachukua hatua

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabia nchi yameleta athari kote ulimwenguni, miongoni mwa changamoto zilizoletwa na adha hiyo ni pamoja na ukosefu wa mvua hali inayopelekea kuwepo na uhaba wa chakula na mahali pengine mvua kubwa zinazosababisha mafuriko na mazao kushindwa kustawi kabisa.

Maeneo yanayokaliwa na wakimbizi pia yanapitia changamoto hii. Makazi ya muda wanayoishi wakimbizi yanashindwa kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi hivyo shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi, mbali na kuhakikisha usalama wao pia linakuja na mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo. Leah Mushi ameangazia wakimbizi wa Ethiopia walioko Sudan na hatua zinazochukuliwa na UNHCR

Soundcloud

 

Video iliyoandaliwa na UNHCR, ambayo imerekodiwa kutoka angani, inaonesha eneo pana, kame, hata huwezi kuona ukijani juu ya ardhi isipokuwa mahema yaliyotapakaa kila mahali.

Wakimbizi wengine wanaonekana wakipanda vilima kuingia hapa na wamebeba virago vyao. Kambini wanaonekana watoto wakiwa na madumu ya maji.

Ethiopia, nchi iliyoko katika pembe ya Afrika, mji wake wa kaskazini, Tigray, ulikumbwa na machafuko na kusababisha maelfu ya wakazi wake kuyakimbia makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR likawapatia hifadhi wakimbizi hawa katika nchi ya jirani, Sudan kwenye makazi ya wakimbizi ya Tunaydbah.

Afisa wa UNHCR Akaran Napakiro katika kambi hii ya Tunaydbah iliyopo Mashariki mwa nchi ya Sudan anasema kama unavyoona eneo hili, ni tambarare isiyo na chochote.

Afisa huyo anaeleza kuhusu idadi ya wakimbizi hawa ambao wamewasili hapa na vifurushi vidogo vya mavazi yao waliyokuwa wameyabeba wakati wa safari yao kukimbia machafuko na sasa wapo kwenye makazi mapya ambapo nyuzi joto lake ni 45 za selisiasi akisema, “idadi ya watu hapa ni takriban elfu ishirini ambao wamekuja hapa na kama asilimia sitini ni vijana na watoto.”

UNHCR kwa kushirikiana na wadau wengine wameleta mbinu mbadala za kimazingira kupambana na hali mbaya ya hewa katika makazi ya wakimbizi. Wanatoa maji, chakula, mavazi, makazi na suluhisho la nishati mbadala. Akaran Naparimo anaeleza kuwa, “wakimbizi wamepokea majiko ya kupikia ambayo ndio wanayatumia kwa sasa na imepunguza gharama za nishati. Tumetoa taa zinazotumia umeme wa jua, taa hizo za jua zitawasaidia wakimbizi kupata mwanga usiku."

Hali mbaya ya hewa imewaacha wakimbizi na jamii zilizowakaribisha wakimbizi hawa katika hali ya hatari. Mvua na upepo mkali hivi karibuni umeharibu nyumba wanazoishi na vyoo wanavyotumia na kuleta mafuriko katika baadhi ya maeneo ya kuishi.

Afisa huyu wa UNHCR anasema wanafanyakazi kuhakikisha wanawalinda wakimbizi kutokana na hatari ya mafuriko, “mikakati ipo ya kuhakikisha tunaweka mifereji ya maji mbali na makazi ya watu”.

Na iwapo mafuriko yatatokea na kuathiri makazi basi kwa kushirikiana na wadau wengine, UNHCR wamejipanga kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi. Bi Naparimo anasema, “tuna vituo vya uokoaji inapotokea baadhi ya makazi ya familia za wakimbizi yameharibiwa, tuna uwezo wa kuwahamisha kwa haraka iwezekanavyo.Tunataka kuunganisha nguvu kazi zote hizi kuhakikisha wakimbizi wapo tayari kukabiliana na mafuriko na kuhakikisha tunajiandaa kukabiliana na changamoto nyingine zitakazojitokeza kwa sababu ya mafuriko, kama vile kipindupindu.”

Kwa sasa Sudan imewapatia makazi wakimbizi zaidi ya milioni moja pamoja na watu walioomba hifadhi, wakiwemo maelfu ya raia wa Ethiopia waliokimbia Tigray pamoja na wasudani milioni mbili wakimbizi wa ndani.

Msimu wa mvua unafanya kufikika kwenye kambi hii kuwa vigumu kutokana na barabara kuharibika vibaya, na kijiji cha karibu na kambi hii kipo umbali wa kilometa 136. Mwaka jana, mafuriko na mvua kubwa zilileta madhari kwa nchi yote ya Sudan na kufanya mamia ya wananchi kukosa makazi ya kuishi.