Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP inatoa msaada wa haraka kwa familia zilizokwama katika mzozo wa Gaza 

Familia zikipokea vifurushi vya chakula Gaza kupitia UNRWA.
UNRWA/Khalil Adwan
Familia zikipokea vifurushi vya chakula Gaza kupitia UNRWA.

WFP inatoa msaada wa haraka kwa familia zilizokwama katika mzozo wa Gaza 

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, WFP limeanza kutoa msaada wa dharura kwa zaidi ya watu 51,000 kaskazini mwa Gaza kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu miongoni mwa familia zilizoathiriwa na kuongezeka kwa mzozo hivi karibuni katika ukanda wa umaskini. 

Katika taarifa iliyotolewa hii leo mjini Jerusalem, WFP imesema kwa kufanya kazi pamoja na wadau wake, shirika hilo linatoa msaada wa pesa ambao utawanufaisha watu wote ambao sasa wanahitaji msaada kwa mara ya kwanza na watu ambao walikuwa tayari wanapokea msaada wa WFP lakini walilazimika kuacha vitu vyao nyuma na kwenda kukaa na marafiki au familia mahali pengine. 

Mwakilishi wa WFP ambaye pia ni Mkurugenzi wa WFP nchini Palestina Samer AbdelJaber amenukuliwa akisema, "kwa watu ambao wamepoteza au kukimbia makazi yao, moja ya mahitaji muhimu zaidi kwa sasa ni chakula. Njia ya haraka na bora zaidi tunaweza kutoa msaada ni pesa taslimu, kwa njia ya vocha za barua pepe. Chakula kinapatikana kwa sasa na maduka mengi ya ndani bado yako wazi, pamoja na yale ambayo tayari tumeingia nayo mkataba kwa ajili ya msaada wetu wa kawaida wa vocha za kielektroniki.”   

WFP inasema kutokana na kufungwa kuvuka kwenda Gaza hivi karibuni kunaweza kusababisha uhaba wa bidhaa, pamoja na chakula, na kupandisha bei za chakula. Bei za mazao mabichi tayari zinaongezeka wakati wakulima hawawezi kufikia ardhi zao. 

Kwa sasa, WFP inafanya kazi na wadau ili kuongeza uratibu, kuanzisha itifaki na kuamua mahitaji ya dharura ya chakula kwa watu wanaotafuta usalama katika makazi ya Umoja wa Mataifa. Njia ya vocha za kielektroniki za pesa za WFP pia zinatumiwa na mashirika mengine ya kibinadamu kutoa mahitaji yasiyo ya chakula pamoja na misaada mingine ya msingi kwa wa walioathirika. 

WFP pia inatoa msaada wa kiufundi kutathmini mahitaji ya kibinadamu huko Gaza na inasaidia kupitia mipango ya usafirishaji zinazoongozwa na WFP, uratibu wa mizigo ya kibinadamu ambayo inaweza kuhitaji kuingia katika eneo hilo ikiwa mipaka itabaki imefungwa. 

WFP inahitaji nyongeza ya Dola za Marekani milioni 31.8 ili kuweza kuendelea kutoa msaada wa kawaida wa chakula kwa watu zaidi ya 435,000 walio katika mazingira magumu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi kwa miezi sita ijayo. Ili kushughulikia dharura ya sasa, WFP inahitaji haraka Dola za Kimarekani milioni 14 kuweza kutoa msaada wa dharura katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa watu 160,000 walioathirika huko Gaza na watu 60,000 katika Ukingo wa Magharibi. Idadi ya watu wanaohitaji inaweza kuongezeka zaidi. 

Kuongezeka mashambulizi ya kijeshi kumesababisha mateso na uharibifu mkubwa. WFP inaomba kuondolewa haraka na kusitishwa kwa uhasama huko Gaza na Israeli.