Idadi ya watoto waliouawa Gaza yafikia 40: Wanane wameuawa usiku wa kuamkia leo 

15 Mei 2021

Watoto wanane wa kipalestina wameuawa usiku wa kuamkia leo huko Ukanda wa Gaza, limesema shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Ted Chaiban amenukuliwa kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Amma, Jordan akisema, “watoto wanane wa kipalestina wameuawa kaskazini mwa Gaza usiku wa kuamkia leo na kufanya idadi ya watoto waliouawa tangu tarehe 10 mwezi huu wa Mei kufikia 40.” 

Umri wa watoto hao ni kati ya miezi 6 hadi miaka 17 ambapo nusu ya hao 40 walikuwa na umri wa chini ya miaka 10. 

Chaiban amesema zaidi ya watu 1,000 huko Gaza wameripotiwa kujeruhiwa, wengine wakiwa na majeraha makubwa wakiwemo watoto. 

Huko Israel nako, watoto wawili, akiwemo mmoja mwenye umri wa miaka 6 wameuawa tangu kuanza mwa mashambulizi kutoka pande zote siku tano zilizopita. 

“Wiki iliypita, huko Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, pamoja na Yerusalem Mashariki mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 16 aliuawa na watoto wengine 54 wa kipalestina walijeruhiwa huku 26 wakitiwa korokoroni. Hata hivyo wengi wao wameshaachiliwa huru,” amesema Mkurugenzi huyo wa UNICEF. 

Uharibifu wa shule 

Shule 35 katika ukanda wa Gaza zimeharibiwa huku shule nyingine zipatazo 29 zikitumika kama makazi ya muda kwa familia ambazo zimekimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya makombora. 

Idadi kubwa ya wakimbizi hao wa ndani 10,000 ni watoto ambapo UNICEF imepokea ripoti kuwa huko Israel shule tatu zimeharibiwa. 

UNICEF inasema kuwa mashambulizi ni makali na watoto ndio wanabeba mzigo mkubwa wa madhara yake, “pande zote zina wajibu wa kulinda raia hususan watoto, na kufanikisha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu. Mzizi wa ghasia hizi hautang’olewa kwa mapigano.” 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter