Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaya zinazoongozwa na mzazi mmoja zimeongezeka- UN

Mume wa Deborah aliuawa siku ambayo alijifungua mtoto wao wa mwisho. Hivi sasa yeye ndiye anayetunza familia yake.
WFP/Gabriela Vivacqua
Mume wa Deborah aliuawa siku ambayo alijifungua mtoto wao wa mwisho. Hivi sasa yeye ndiye anayetunza familia yake.

Kaya zinazoongozwa na mzazi mmoja zimeongezeka- UN

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya familia, Umoja wa Mataifa unaangazia umuhimu wa teknolojia katika kuimarisha ustawi wa taasisi hiyo muhimu kwa maendeleo endelevu duniani.

Kupitia wavuti mahsusi wa siku hii Umoja wa Mataifa unasema, "mienendo mipya, zikiwemo teknolojia, mabadiliko ya makundi ya kijamii na watu, kasi kubwa ya kukua kwa miji na uhamiaji sambamba na mabadiliko ya tabianchi, vinaleta mabadiliko makubwa kwenye dunia yetu."

Kama hiyo haitoshi, uwepo kwa muda mrefu kwa janga la Corona au COVID-19, umedhihirisha umuhimu wa teknolojia za kidijitali kwa ajili ya kazi, elimu na mawasiliano.

Mwabamke aliyefurushwa akiwa amekaa na familia yake kwenye hema katika kituo cha makazi ya waliofurushwa, Palma, jimbo la Cabo Delgado.
© WFP/Grant Lee Neuenburg
Mwabamke aliyefurushwa akiwa amekaa na familia yake kwenye hema katika kituo cha makazi ya waliofurushwa, Palma, jimbo la Cabo Delgado.

"Janga la Corona limechochea kasi ya mabadiliko ya teknolojia ambayo tayari yalishaanza kuwepo ikiwemo kupanuka kwa matumizi ya majukwaa ya kidijitali," umesema Umoja wa Mataifa.

Ni kwa kutambua hilo, kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya mwaka wa familia ifikapo mwaka 2024, Umoja wa Mataifa unalenga kuongeza uelewa wa mienendo mikubwa hiyo ya mabadiliko duniani na kuibuka na sera za kuchukua hatua zinazojali familia.

Familia zinabadilika

Ulimwenguni kote muundo wa familia unabadilika, nyingine zinakuwa kubwa, mathalani kaya zinazoongozwa na mzazi mmoja zinaongezeka.

HIvi sasa asilimia 65 ya familia zote zinaundwa na wanandoa wanaoishi na watoto wenye umri mbalimbali, au wanandoa wanaoishi na watoto na jamaa, kama vile babu na bibi.

Kupungua kwa idadi ya familia zinazoishi na jamaa na ongezeko la familia zinazoongozwa na mzazi mmoja, kunaweka msisitizo wa umuhimu wa suala la hifadihi ya jamii.

Mchakato wa siku ya familia ulianza lini?

Wakati wa miaka ya 1980, Umoja wa MAtaifa ulianza kumulika suala la familia na mwaka 1983 kwa kuzingatia pendekezo la Baraza la Uchumi na Kijamii la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipitisha azimio la kumuomba Katibu Mkuu aongeze uhamasishaji na uelewa kwa wapitisha maamuzi juu ya changamoto na mahitaji ya familia pamoja na hatua bora za kuinusuru.

Baada ya mchakato, tarehe 9 Desemba mwaka 1989, Baraza Kuu lilitangaza kuwepo kwa mwaka wa familia na kisha mwaka 1993 kupitia azimio namba 47/237 liliamua tarehe 15 mwezi Mei kila mwaka kuwa siku ya familia.

Siku hii inatoa fursa ya kujadili na kusongesha masuala yanayohusu familia na kuongeza uelewa wa michakato ya kiuchumi, kijamii na kidemografia ambayo inaathiri familia.