Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde waisrael na wapalestina, suluhu ni la kisiasa pekee na si mtutu: Guterres

Nyumba zimesambaratishwa kwa makombora huko Ukanda wa gaza kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya wapalestina na waisrael
UNOCHA
Nyumba zimesambaratishwa kwa makombora huko Ukanda wa gaza kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya wapalestina na waisrael

Chonde chonde waisrael na wapalestina, suluhu ni la kisiasa pekee na si mtutu: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano mara moja huko Ukanda wa Gaza na Israel.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa leo jijini New York, Marekani akimnukuu Katibu Mkuu akisema, "mapigano yanayoendelea yanasababisha machungu makubwa na uharibifu. Yameua raia, wakiwemo watoto. mapigano haya yanaweza kuiua janga kubwa la ukosefu wa usalama na janga la kibinadamu na kuchochea misimamo mikali, siyo tu kwenye maeneo ya wapalestina yanayokaliwa na Israel bali pia Israel na ukanda mzima wa Mashariki ya Kati."

Katibu Mkuu ametaka pande hizo ziruhusu jitihada za usuluhishi zenye lengo la kumaliza mapigano hayo mara moja.

Bwana Guterres amesema Umoja wa Mataifa unashiki kikamilifu katika juhudi hizo ambazo ni muhimu pia ili mahitaij ya kibinadamu yanayohitajika yaweza kuwafikia wakazi walioathirika huko Gaza.Amesisitiza kuwa suluhisho la kisiasa ndio linaloweza kuleta amani ya kudumu na kwamba, "nasisitiza azma yangu katika juhudi ikiwemo kupitia mpango wa pande nne wa kusaka suluhu ya kudumu Mashariki ya Kati ili hatimaye wapalestina na waisrael wasuluhishe mgogoro wao kwa kutumia maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya pande mbili."

Tweet URL

Guterres ataka Eid iheshimiwe

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia mtandao wake wa Twitter ametuma salamu za Eid na kuhimiza kusitishwa kwa mapigano yanayoendelea katika ukanda wa Gaza.

Amesema "kwa kuheshimu sikukuu ya Eid nawasihi kusitisha mapigano kwani yanaongeza uhasama baina ya upande wa Gaza na Israel. Watu wengi wasio na hatia wamepoteza maisha, na mapigano haya yanaongeza uhasama na chuki kali katika eneo hilo"

Hali ya kibinadamu ni tete - OCHA

Nayo taarifa kutoka Geneva Uswisi kwa msemaji wa ofisi ya umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu OCHA, Jens Laerke, imesema idadi ya raia walioathirika na mapigano hayo imeongezeka mara dufu huku zaidi ya majengo 200 ya raia na shule 31 zikiharibiwa na makombora yanayorushwa.

Mamia ya wakimbizi waliopo katika kambi huko Gaza wanakimbilia kuomba hifadhi katika shule sinazosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, ( UNRWA)

"UNRWA imeshuhudia namna shule zilivyogeuzwa makazi ya wanaoomba hifadhi kwa kasi sana lakini changamoto ni janga la covid19 na ongezeko hili la watu linaweza ongeza maambukizi ya virusi vya Corona. Lakini pia tunashindwa kuandaa makazi vyema kutokana na wafanyakazi wetu kuzuiwa kutembea kwa siku mbili zilizopita." Amesema Bwana Laerke.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa OCHA, athari kubwa zinazoletwa na mapigano hayo ni pamoja na uvuvi kusimama katika pwani ya Gaza, upungufu mkubwa wa mafuta ya kuendesha mitambo ambapo kama hali haitatengemaa ndani ya siku chache zijazo huduma muhimu ikiwemo maji na umeme zitaathirika na kuleta madhara katika utoaji huduma za afya na maji safi na salama.