Wananchi Guinea wahofia wagonjwa wa Ebola kunyofolewa viungo, WHO yachukua hatua 

14 Mei 2021

Nchini Guinea shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limezindua mpango wa pamoja na serikali wa mawasiliano kwa lengo la kukabili kusambaa kwa habari potofu dhidi ya ugonjwa wa Ebola, ikiwemo uvumi ya kwamba miili ya watu wanaofariki dunia kutokana na ugonjwa huo inatolewa viungo vyao kwa ajili ya biashara.

Dkt. Julienne Anoko, Mratibu wa WHO nchini Guinea, amesema uvumi umeenea zaidi jimbo la N’zerekore ambako pia jamii inakumbwa na uvumi ya kwamba wahudumu wa afya wanachukua damu za wagonjwa kwa shughuli za kiuchawi. 

Ni kwa mantiki hiyo, mpango huo wa mawasiliano anasema “unawawezesha kufanya pamoja juhudi zao WHO na serikali kukabili uvumi na taarifa potofu na kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopaswa kufikiwa na taarifa yanaguswa ili kuepusha kusambaa zaidi kwa Ebola.” 

Mkakati unahusisha vikao na wanajamii, viongozi wa kikabila na kidini na wataalamu wa masuala ya kijamii. 

Dkt. Anoko anasema, “wakati wa janga, watu wanapata hofu. Na pindi wanapokuwa na hofu na hawapati taarifa nzuri na sahihi, watakuwa na mbinu zao za kutafsiri kile kinachoendelea ambapo uvumi ni miongoni mwa mbinu hizo.” 

Hofu imekuwa jambo linalozingira virusi vya Ebola na uvuvi hatari ulioambatana nao ni sehemu ya kumbukumbu ya Ebola tangu wakati wa mlipuko wa mwaka 2014 hadi 2016 ambapo zaidi ya watu 11,000 nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia walifariki dunia. 

Mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini Guinea kwa mwaka huu alibainika tarehe 14 mwezi Februari na hadi sasa wagonjwa wamefikia 23 na kati yao hao 12 wamefariki dunia. 

Wadau katika kampeni hiyo ya kukabili uvumi na habari potofu wakati wa mlipuko wa sasa wa Ebola nchini Guinea ni pamoja na shirka la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, shirikisho la kimataifa la msalaba mwekundu, IFRC na WHO. 

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni WHO Guinea kuandaa ripoti ya kila wiki ya taarifa za kwenye mitandao ya kijamii ambayo wanapatia pia wadau wao. 

Ripoti hiyo inawezesha wadau hao kuandaa ujumbe unaolenga kukabili uvumi na taarifa potofu zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na ujumbe huo unasambazwa kupitia mitandao ya kijamii na radio kwa kuzingatia kuwa bado radio inatumika zaidi na intaneti inafikia asilimia 21 tu ya wananchi wa Guinea na ni asilimia 15 tu ndio wako kwenye mitandao ya kijamii. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter