Guterres akutana na Rais Putin mjini Moscow na kuzungumza na wanafunzi MGIMO

13 Mei 2021

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye yuko ziarani mjini Moscow, amefanya mkutano wa kawaida na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Viongozi hao wawili wamesisitiza haja  ya kujikita na ahadi ya mshikamano wa kimataifa na ushirikiano, ambao wanaamini utasaidia jamii ya kimataifa kukabiliana na changamoto kubwa kama janga la corona au COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi. 

"Wamejadili masuala kadhaa ya kimataifa na ya kikanda katika upande wa amani na usalama, pia katika upande wa masuala ya ya kibinadamu, na hitaji la kusuluhisha mizozo kupitia mazungumzo ya kisiasa, kuonyesha kuheshimiana na kuelewana," imesema taarifa ya Katibu Mkuu iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani. 

Katibu Taarifa hiyo imeendelea kusema Bwana Guterres ametia msisitizo katika maeneo matatu ambayo ndio yanayounda msingi wa kazi ya Umoja wa Mataifa na maeneo hayo ni amani na usalama, maendeleo endelevu, ikiwemo kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi bioanuwai, na haki za binadamu. 

Katibu Mkuu amemshukuru Rais Putin kwa ukarimu na kwa msaada ambao Urusi inaendelea kuutoa kwa Umoja wa Mataifa. Pia amewapongeza watu wa Urusi katika Siku ya Ushindi waliopupata miaka ya nyuma. 

Azuru taasisi ya MGIMO 

LSiku ya leo pia, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametembelea taasisi ya uhusiano wa Kimataifa ya Jimbo la Moscow (MGIMO) na kuzungumza na wanafunzi wake kuhusu shida na changamoto zinazoikabili jamii ya kimataifa hii leo.  

Katibu Mkuu amehutubia wanafunzi na washiriki wa Umoja wa Mataifa wa mfano (Model UN), ambao walikuwepo kwenye ukumbi huo, ambao wanatatua changamoto za kimataifa kwa kufuatia mfano wa Umoja wa Mataifa na vyombo vyake.  

Taasisi ya MGIMO, ni mradi uliopewa jina la Vitaly Churkin, ambaye tangu 2006 hadi kifo chake mnamo mwaka 2017 alikuwa mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa.  

Antonio Guterres amesisitiza kuwa Churkin alikuwa mwanadiplomasia wa kipekee ambaye alijitolea kukuza maadili ya Umoja wa Mataifa.  

Kwa uamuzi wa Baraza la Taaluma la Chuo Kikuu hiocho, Guterres ametunukiwa shahada ya daktari wa heshima wa MGIMO "Kwa mchango wake bora katika uimarishaji wa amani, ushirikiano wa kimataifa na uhusiano wa kirafiki kati ya watu."  

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa pia alikutana huko Moscow na Balozi mwema wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Arctic na Antarctic, ambaye ni mchezaji maarufu wa mpira wa magongo au Hockey, Vyacheslav Fetisov. Mwanamichezo huyo alimpa Guterres jezi binafsi ya mpira wa magongo. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter