Hospitali bila wauguzi ni sawa na gari bila injini – Muuguzi Mildred Okemo

12 Mei 2021

Ikiwa leo ni siku ya wauguzi duniani, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linasema, licha ya jukumu muhimu wanalofanya wauguzi  katika huduma ya afya, kuna uhaba wa wafanyakazi hao ulimwenguni, uhaba ambao unatarajiwa kuongezeka kadiri idadi ya watu inavyoongezeka.

WHO inaeleza kuwa wauguzi wana jukumu muhimu katika huduma za afya na mara nyingi ni mashujaa wasiojulikana katika vituo vya huduma za afya na huduma za dharura. Mara nyingi wao ndio wa kwanza kugundua dharura za kiafya na hufanya kazi katika mstari wa mbele kuzuia magonjwa na utoaji wa huduma ya msingi ya afya, ikiwemo kukuza afya, kuzuia maginjwa, na kutibu. 

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa wauguzi na wakunga ni takribani asilimia 50 ya wafanyakazi wa afya ulimwenguni lakini pia wanawakilisha asilimia 50 ya uhaba wa wahudumu wa afya ulimwenguni, pengo ambalo linakadiriwa kuwa la wauguzi milioni 4 na ili kufikia lengo la huduma ya afya kwa wote itahitaji juhudi kubwa kupunguza uhaba wa wafanyakazi wa afya ulimwenguni. 

Mildred Okemo ni muuguzi anayehudumu katika hospitali kuu ya Valley, kwenye jimbo la New Jersey Marekani. Muuguzi huyu anaunga mkono wito wa WHO wa kuongeza idadi ya wauguzi akisema,"siku hii ni ya muhimu sana hasa kufuatia janga la Covid-19 ambalo limedhihirisha umuhimu wa kazi yetu. Ninawapongeza wauguzi wote na kuitaka jamii kuunga mkono kazi yao kwani inaokoa maisha. Hospitali bila wauguzi, ni sawa na gari bila injini."

Muuguzi Mildred anasema kazi ya uuguzi ina changamoto, lakini kuna kinachompa motisha ya kuendelea,

"changamoto kati hii kazi ni kuwa kazi yenyewe ni hatari katika maambukizi ya ugonjwa kazini na hata kuambukiza jamii nyumbani. Kinachonipa motisha kuendelea na hii kazi ni kuwa wagonjwa wanapopona wananipa shukrani, na zaidi ya yote ni neema ya Mungu."

Siku ya wauguzi duniani, huadhimishwa tarehe 12 Mei kila mwaka, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taaluma hii ya uuguzi wa kisasa, Florence Nightingale ambaye angekuwa anatimiza miaka 201 hii leo.  

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter