Hali ya njaa Madagascar ni tete! UN na serikali wataka msaada wa haraka 

12 Mei 2021

Msaada wa kibinadamu wa haraka unahitajika ili  kuwanusuru wananchi waishio kusini mwa Madagascar ambao sasa wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame ulioikumba nchi hiyo. Mashirika mawili ya umoja wa mataifa kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo wametoa wito huo wakati huu ambapo takribani watu milioni 1.4 kusini mwa nchi hiyo hawana uhakika wa mlo wao huku watoto wakiendelea kupoteza maisha.

Kijiji cha SIHANAMARO kusini mwa Madagascar, Si wazee wala watoto, wote wamelegea hawana chakufanya , wazazi nao hawajui namna gani ya kuwaondoa watoto wao kwenye hali hii kilichobaki ni kuwaweka vizuri na kuwapa moyo wawe na matumaini pengine mambo yatakuwa mazuri. 

Wote hawa wanakabiliwa na njaa … njaa ambayo kama haitatatuliwa basi takwimu zinasema kufikia mwezi Oktoba mwaka huu mambo yatakuwa mabaya zaidi.  

Pengine wangetamani kulima ili waweze kujikwamua katika baa hili lakini mabadiliko ya tabia nchi yaliyoleta ukame mkali kupata kutoeka ndani ya mionngo minne yamewafanya kupoteza matumaini kabisa. ….  

Hali hii ndio imesababisha mashirika mawili ya umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo duniani- FAO na la Mpango wa chakula duniani – WFP kwa kushirkiana na serikali ya Madagascar kuomba msaada wa haraka wa kibinadamu kusaidia wananchi hawa wa kusini mwa nchi hiyo. 

Mkurugenzi mwandamizi wa operesheni za  WFP nchini humu, Amer Daoudi  amesema “ Suala sio hali ni mbaya kiasi gani tena, maana ni mbaya sana. Watoto wana njaa kali, watoto wanakufa. Nimekutana na mama mwenye mtoto wa umri wa miezi minane lakini anaonekana kama ana umri wa miezi miwili, mama huyu tayari mtoto wake mwingine mkubwa ameshafariki. Tunaona namna ambavyo watu wanakimbia baa hili la njaa na kukimbilia mjini na hii inaongeza tatizo jingine.” 

Suala la msaada wa kibinadamu nila haraka ili kuokoa maisha ya watu lakini pia Mkurugenzi wa masula  ya dharura wa FAO Dominique Burgeon amegusia ukame mkali uliosababisha  njaa kwa asilimia 95 ya wakazi wa kusini na  kutoa wito kwa wadau kutupia jicho misaada ya kilimo na mifugo. 

Anasema, “ lazima tuchukue hatua za dharura ya kuilinda mifugo isife na kuwapatia mbegu , vifaa vya umwagiliaji na ufugaji ili kuinua uzalishaji wa chakula katika eneo hili, lakini pia hatuwezi kufumbia macho uhitaji wa kujikita kwenye kilimo cha kukabiliana na mabdiliko ya tabianchi kwa mstakabali wa maisha yao ya muda mrefu. 

Kazi ya ugawaji wa chakula imekuwa ngumu na kushindwa kufanyika kwa haraka kutokana na changamoto za ugonjwa wa Corona au COVID-19, ambapo ndege zimeshindwa kutua katika kisiwa hiki na hivyo namna pekee kufikisha msaada ni kwa kutumia boti, hali inayofanya mgao kuwa kidogo ikilinganishwa na uhitaji. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter