Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili wa Benki ya dunia kwa nishati ya jua, nuru kwa wafanyabiashara Somalia

Watu wakiweka paneli za nishati ya jua.
UNDP Yemen
Watu wakiweka paneli za nishati ya jua.

Ufadhili wa Benki ya dunia kwa nishati ya jua, nuru kwa wafanyabiashara Somalia

Wahamiaji na Wakimbizi

Kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia kwa Mfuko wa Kichocheo cha Biashara Somalia, SBCF, kampuni ya Solargen kupitia umeme wa nguvu ya jua imefanikiwa kuleta unafuu wa kimaisha kwa wananchi wa Warsheikh, katika pwani ya Somalia.

Mtu mmoja kati ya watu watatu nchini Somalia, ndiye ana uwezo wa kupata umeme, ikilinganishwa na takribani nusu ya waafrika wengine kusini mwa jangwa la Sahara. Hali hii inamaanisha kuwa biashara nyingi zinategemea jenereta za gharama zinazotumia dizeli  ili kuendesha shughuli za kila siku. Makampuni kama Solargen yanasaidia kushughulikia changamoto hizo kwa njia ambayo ni rafiki kwa mazingira na pia ni bei nafuu, nguvu ya jua. Mohamed Abukar Adaawe ni mfanyabiashara nchini Somalia anasema, “biashara katika mji wa pwani wa Warsheikh umeshuhudia mabadiliko makubwa kati ya zamani na sasa. Zamani tulikuwa tunatregemea jenereta kwa ajili ya kupata umeme. Umeme ulikuwa unapatikana kwa ajili ya matumizi kati ya sita mchana hadi saa tano usiku tu. Katika muda huo hatuweza kuwasha friji, mashine za kufulia nguo au kingine chochote.” 

Solargen inawawezesha wajasiriamali kupunguza gharama zao na kupanua biashara zao kama anavyothibitisha mfanyabiashara Adaawe ambaye anasema, “hivi sasa kwa msaada wa paneli za sola tunatumia dola 10 tu za kimarekani kwa mwezi, kwa ajili ya umeme ambao unakuwepo saa 24, siku 7 za wiki. Na kutokana na akiba ambayo inabaki, nimeweza kufungua duka jingine. Bila mpango huu kutoka Solargen, nisingeweza kubaki katika biashara.” 

Benjamin Musuku, Mratibu wa programu ya sekta ya Benki ya dunia katika Somalia anasema, “faida kubwa muhimu ya mradi ni kuwa tumeweza kutengeneza zaidi ya kazi mpya 2,200 kutokana na biashara zilizosaidiwa. Sekta tatu kubwa ambazo zilichangia katika ukuaji wa kazi ni uzalishaji viwandani, zaidi ya kazi 620, kilimo, zaidi ya kazi 300, uvuvi, zaidi ya kazi 330.”  

Kwa ujumla, wakazi wa mji wa pwani wa Warsheikh, wanasema mradi wau meme nafuu unaotumia nishati ya jua, umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao na sasa wanashuhudia ukuaji wa mji wao, hotel zinajengwa, na watalii, wameanza kumiminika.