Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanamke mtengeneza juisi Uganda aangukiwa na nuru na sasa ana maono makubwa

Wafanyakazi  wa kampuni ya juisi ya Cheers wakiwa na Julian Omalla (katikati) karibu na shamba lenye tunda yanayotumika kutengeneza rojo au juisi ya kampuni hiyo.)
Delight Uganda Limited
Wafanyakazi wa kampuni ya juisi ya Cheers wakiwa na Julian Omalla (katikati) karibu na shamba lenye tunda yanayotumika kutengeneza rojo au juisi ya kampuni hiyo.)

Mwanamke mtengeneza juisi Uganda aangukiwa na nuru na sasa ana maono makubwa

Wanawake

Julian Omalla ambaye alitinga fainali za kinyang’anyiro cha tuzo ya wanawake wajasiriamali ilyoandaliwa na kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD amekabidhiwa na serikali ya nchi yake Uganda mkopo nafuu wa dola milioni 10 ili ajenge kiwanda endelevu cha kutengeneza juisi.

 

Mjasiriamali Julian Omalla wa nchini uganda, anajivunia biashara ya kutengeneza juisi bora akiwa na zaidi ya wateja milioni 5
Delight Uganda Limited
Mjasiriamali Julian Omalla wa nchini uganda, anajivunia biashara ya kutengeneza juisi bora akiwa na zaidi ya wateja milioni 5

Fedha hizo zitamwezesha kujenga kiwanda kitakachoendelea kilimo endelevu na kuboresha mbinu za watu kujipatia kipato.

Julian Omalla huzalisha moja wapo ya juisi maarufu sana nchini Uganda, ikiuzwa kwa jina la kibiashara "Cheers" ikiwa na wateja wa kutegemewa zaidi ya milioni 5.

Akijulikana sana kama "Mama Cheers", mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 56 ambaye ni mwanzilishi na pia Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Delight Uganda Limited ni miongoni mwa wanawake wajasiriamali maarufu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika kumpongeza kwa uzoefu wake wa muda mrefu na mafanikio katika sekta hiyo, serikali ya Uganda ilimpatia jumla ya dola milioni 10, ikiwa ni mkopo nafuu, ambapo kati ya hizo dola milioni 4 alipatiwa mwezi Februari mwaka huu ili ajenge kiwanda cha juisi kaskazini mwa Uganda.

Halikadhalika, alipatiwa tena na serikali dola milioni 6 kwa ajili ya kununua vifaa, huku asilimia 50 ya fedha hizo zikiwa ni za kulipwa katika kipindi cha miaka 10.

Mafanikio mapya

Mkopo huo nafuu, ni mafanikio mapya katika kikapu cha Bi. Omalla. Yeye ni miongoni mwa wanawake wajasiriamali walio maarufu nchini Uganda, akiwa tayari ametunikiwa tuzo za nchini mwake na kimataifa.

Mwaka jana, alishinda tuzo maalumu katika awamu ya saba ya tuzo za wanawake wajasiriamali za UNCTAD ziitwazo Empretec Women in Business Awards kutokana na kujitoa kwake katika kuwezesha wanawake wenzake kupitia biashara jumuishi.

Tuzo hizo zinatambua mchango wa mafunzo yaliyotolewa chini ya mpango wa UNCTAD uitwao Empretec na kusherelekea mafanikio katika biashara zao.

Tuzo hizo zilifadhiliwa na mradi jumuishi wa Business Action Network, wa shirika la Ujerumani la GIZ.

Bi. Omalla pia alipata ufadhili wa kushiriki kwenye mradi wa elimu ya kiutendaji kwenye chuo cha kimataifa cha usimamizi wa maendeleo huko Lausanne, nchini Uswisi.

Matunda kutoka shambani kama vile maembe hununuliwa kutoka kwa wakulima nchini Uganda badala ya kuagizwa kutoka nje.
Delight Uganda Limited
Matunda kutoka shambani kama vile maembe hununuliwa kutoka kwa wakulima nchini Uganda badala ya kuagizwa kutoka nje.

Awezeshwa na pia kupikwa

"Empretec iliniwezesha na kunifunza au kunipika hadi niwe kile nilicho leo," Bi. Omalla asema.

Alipoanzisha kampuni yake mwaka 1996, hakufahamu mengi kuhusu uendeshaji wa biashara. Mnamo 2000, Empretec ilimpatia ujuzi wa mjasiriamali bora. "Mafunzo yalinisaidia kutambua kwamba nilizaliwa nikiwa mjasiriamali," akumbuka. "Ilinisaidia kuanzisha na kutekeleza mpango wangu wa kibiashara."

Katika miaka iliyofuata, aliendelea kujifunza kutoka wakufunzi wa Empretec na kukuza ujasiriamali wake huku biashara ikinoga. "Niliendelea kuuliza maswali kuona kwamba nimeimarisha biashara yangu, hata wakati wa mwishoni wa juma,"anasema.

Kwa miaka zaidi ya 20, Charles Ocici, Mkurugenzi wa Empretec katika kampuni ya Enterprise Uganda, amemfundisha na kuelekeza Bi. Omalla kuhusu jinsi gani ya kuwa mjarsiriamali bora zaidi. "Imekuwa furaha kwangu kumfundisha katika safari yake ya kijasiriamali," asema Bwana Ocici. "Alijenga msingi mkubwa chini."

Omalla amesema Empretec ilimfanya ajiamini katika ujasiriamali wake kama vile kujiwekea malengo, kuweka rekodi za kifedha, uuzaji na utangazaji wa bidhaa na kuchapa kazi kwa dhati ili atimize malengo yake.

Uzalishaji wa lita 12,000 kwa siku

Na ujuzi kutoka Empretec na bidii yake, Bi. Omalla alikuza kampuni hiyo ndogo hadi kiasi cha kuwa na asilimia 60 ya mgao sokoni akiwa kileleni baada ya kujenga mtambo unaosindika na kuzalisha lita 12,000 za juisi zenye ladha ya matunda kwa siku.

Bi. Omalla alishinda changamoto nyingi akiendelea ambazo ni pamoja kukwama kabisa baada ya mshirika wake wa biashara kukimbia na sehemu ya mtaji. "Kawaida huwa najifunza kutokana na changamoto zinazonikabili au ninaposhindwa. Sikuwahi kukubali changamoto zinikwamishe kabisa," asema.

Kupata fedha za kupanua biashara yake ilikuwa changamoto kubwa, kama wanawake wengine nchini Uganda, hakuwa na rasilimali ambazo hupendwa na benki kama dhamana kabla ya kufadhili biashara ya mtu. Alikuwa anategemea fedha anazoweka na kuwekeza faida za mapato yake katika biashara ili ipanuke. Pia aliwekeza kwenye bishara zingine kama ufugaji, kuuza mandazi na kusagisha unga.

"Cheers" ni moja ya juisi maarufu kutoka kampuni ya Delight Uganda Limited
Delight Uganda Limited
"Cheers" ni moja ya juisi maarufu kutoka kampuni ya Delight Uganda Limited

Kubadili ndoto kuwa mafanikio

Hadi 2011, Bi. Omalla alikuwa akizalisha "Cheers" akitumia malighafi za kutengeneza juisi zilizonunuliwa kutoka nje ya Uganda, kwa kiasi fulani kutokana na changamoto ya nyenzo za kiwango kikubwa zaidi na matunda yaliopandwa na wenyeji.

Kisha alianza kutekeleza ndoto yake ya muda mrefu ya kuzalisha juisi kwa kupata ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,700 kwa ajili ya kupanda miti ya matunda, kama maembe, mapera na karakara.

Alianza kukuza miche ili apate matunda bora na akaendelea chini ya chama cha ushirika, wakulima 5,000 wa matunda waliokuwa na mikataba ya kuzalisha mazao kwa ajili ya viwanda katika wilaya ya kaskazini mwa nchi ya Nwoya.

Kati ya wanachama wake 5,000, kundi la chama cha ushirika cha wakulima cha Nwoya kulikuwepo wanawake 3,750 wakulima wa matunda ya kutumiwa na kampuni ya Delight Uganda, ikinufaisha wanawake zaidi ya 100,000 moja kwa moja au kwa njia zisizo za moja kwa moja.

Bi. Omalla, alichagua jina "Cheers" na biahsara yake kwani linaonesha ubora wa kazi. Yeye ni kiongozi kielelezo, anayetia moyo, mhamasishaji, na kuajiri watu wa tabaka mbalimbali hasa wanawake waliohatarini wanaopambana kutafuta pato ili wakidhi mahitaji ya familai zao.

Ili kuimarisha usalama wao wa kifedha, alihakikisha kwamba kila mwanamke katika shirika anakuwa na angalau ekari moja ya matunda na matunda ya muda mfupi kwa ajili mapato endelevu. Kila mkulima anaweza kupata dola 1,850 kila msimu kutoka kwenye ekari moja ya ardhi.

Aina za juisi zinazotengenezwa na mjasiriamali Julian Omalla ambaye alishinda tuzo ya UNCTAD
Delight Uganda Limited
Aina za juisi zinazotengenezwa na mjasiriamali Julian Omalla ambaye alishinda tuzo ya UNCTAD

Kazi za kusaidia jamii

"Mama Cheers" pia amesaidia kuwapatia ujuzi wanajamii kupitia taasisi ya shamba la Delight, akisaidia kuleta kazi mpya na bora huku ukileta pato kwa watu wengi sana.

Wakiwa na matunda bora na mbegu za mafuta jamii ilipata fursa ya kuimarisha lishe. Hili lilifuatwa kuimarishwa kwa miundombinu kama barabara, ambazo hurahisisha wakulima kufikia masoko.

COVID-19 na kuoza kwa matunda

Kutokana na vikwazo vya kudhibiti COVID-19 nchini Uganda, ikiwemo vile vya kuzuia usafirishaji wa bidhaa, matunda yaliivia shambani na kuoza na hiyo kusababisha hasara kubwa. Matunda yalikuwa hayawezi kusafirishwa hadi kwenye hifadhi au masokoni.

Bi. Omalla alitumia fursa hii kuimarisha usimamizi wa shamba kwa ajili ya uzalishaji zaidi akijiandaa kwa muda baada ya vizuizi vya COVID-19. Pia alisambaza miche ya matunda, buni na mihogo katika jamii.

Kiwanda kipya na anga jipya

Kupigwa jeki ya dola milioni 10 na serikali ya Ugandan itasaidia Delight Uganda kujenga kiwanda cha juisi kitakachoongeza thamani ya matunda yanayopandwa na wakulima wa kienyeji n kufungua fursa mpya kwao.

"Tukiwa na kiwanda hiki, tunatarajia kupanua uzalishaji wetu hadi kwenye pembe zote za dunia," asema Bi Omalla. Mpango wake wa muda mrefu ni kukidhi mahitaji ya soko kwa kukausha matunda haya hasa maembe.

Pia anapanga kufanya tasisi ya kufundisha kazi zake ili watu wajifunze kulima mazoa bora, na wawekezaji watakuja kuongeza thamani kwneye matunda.

"Mama Cheers" pia analenga kuongeza idadi ya wakulima wa kujitegemea au "outgrowers" hadi wakulima 80,000 na wanufaika wasio wa moja kwa moja hadi 432,000 katika miaka mitatu ijayo.

Hiki kitasaidia kuhakikisha uzalishaji endelevu kwa kiwanda kipya ili jukidhi mahitaji ya ndani, kikanda na kimataifa.