Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yakaribisha maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya Argania 

Mafuta ya Argan yanajulikana kwa matumizi yake ya upishi na kwa ajili ya mwili kama vile ngozi na nywele.
© Oliver Migliore
Mafuta ya Argan yanajulikana kwa matumizi yake ya upishi na kwa ajili ya mwili kama vile ngozi na nywele.

FAO yakaribisha maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya Argania 

Utamaduni na Elimu

Leo ni maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya Argania mmea wa kipekee unazotumiwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengeneza mafuta ya ogani nchini Morocco.  

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limekaribisha maadhimisho hayo na hususan azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa kuidhinisha Mei 10 kuwa siku ya kimataifa ya Argania likisema limetambua umuhimu wa mmea huo kwa masuala ya bayoanuai, mabadiliko ya tabianchi na mchango wake wa kiuchumi sio kwa Morocco tu unakozalishwa bali pia duniani kote mazao yake yanakouzwa. 

Azimio la siku hii liliwasilishwa na serikali ya Morocco, lilidhaminiwa nan chi wanachama wa Umoja wa Mataifa 113 na kupitishwa nao kwa kauali moja. 

Umuhimu wa mmea wa Argania 

 

Mwezi Desemba mwaka 2018 FAO ilitambua mfumo wa ufugaji na kilimo wa Argan-sylvo ndani ya eneo la Ait Souab - Ait Mansour nchini Morocco kama “Mfumo wa Urithi wa kilimo muhimu duniani , jimbo la kipekee ambako miti ya argan imekuwa ikilimwa kwa karne nyingi.” 

Mfumo wa kilimo misitu na ufugaji huko Ait Souab-Ait Mansour una mandhari bora ambayo inachanganya bioanuai za kilimo, mifumo ya ikolojia yenye mnepo na urithi wa kitamaduni wenye thamani. 

FAO inasema “Jamii za asili za Amazigh na jamii zenye asili ya Kiarabu zimekuza utamaduni na utambulisho maalum, zikishirikiana maarifa na ujuzi wao wa jadi. Ingawa wakulima wanapata mapato yao mengi kutokana na kilimo cha miti ya argan, mfumo huo jumuishi pia huwapatia chakula na nyenzo zingine kama mazao ya chakula kikuu, nafaka, kuni, nyama na sufu.” 

Msisitizo wa azimio la siku hii 

 

Rasimu ya azimio lililowasilishwa na Morocco lilisisitiza jinsi gani sherehe za kila mwaka Mei 10 zitakavyozingatia chanzo cha urithi wa kilimo wa tangu enzi za mababu, kama inavyotambuliwa na programu ya FAO ya GIAHS. 

"Uzalishaji wa mafuta ya Argan huko Morocco na nchi zingine, unaonaendeshwa kimsingi kwa kiasi kikubwa na wanawake, unastahili kupewa uzitio huu, ikiwa ni pamoja na jukumu lake katika kutimiza malengo ya maendeleo Endelevu. Kwa kuashiria siku hiyo, Umoja wa Mataifa utaheshimu jukumu la wanawake, wakulima na wajasiriamali ”imesema taarifa ya FAO. 

Azimio hilo pia linahusiana na shirika laelimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambalo mwaka 2014 liliainisha ujuzi wote kuhusu mti wa argan kama urithi wa kitamaduni usiogusika wa ubinadamu. 

Azimio hilo linatambua mali nyingi za mafuta ya argan, haswa katika dawa za jadi na nyinginezo na katika tasnia ya upishi na mapambo.  

FAO pia inasisitiza jinsi vyama vya ushirika na mashirika mengine ya kijamii ya kilimo yanayofanya kazi katika zao la argan kuwa ni muhimu katika kukuza fursa za ajira za eneo husika.  

Mashirika haya yanaweza kuchukua jukumu muhimu katika kuchangia uhakika wa chakula, kutokomeza umaskini na kuchangia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.