Ninawasihi Israeli sitisheni kinachoendelea mashariki mwa Jerusalem – Antonio Guterres  

9 Mei 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameelezea "wasiwasi wake mkubwa juu ya vurugu zinazoendelea Jerusalem Mashariki, na vile vile uwezekano wa kufukuzwa kwa familia za Wapalestina kutoka kwenye makazi yao katika maeneo ya Sheikh Jarrah na Silwan. 

Katika taarifa iliyotolewa jioni hii, Jumapili, kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, Bwana Guterres amehimiza, "Israeli isimamishe ubomoaji na uhamishaji watu kulingana na wajibu wake chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu." 

Aidha Bwana Guterres amesema Mamlaka za Israeli zinapaswa kujizuia kabisa na kuheshimu haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani. 

Pia akatoa wito kwa viongozi wote "kuchukua jukumu la kuchukua hatua dhidi ya wenye msimamo mkali na kusema dhidi ya vitendo vyote vya ghasia na uchochezi." Katika taarifa yake, Katibu Mkuu alihimiza  na pia "kuzingatia na kuheshimu hali ilivyo katika maeneo matakatifu." 

Maamuzi ya kimataifa na suluhisho la mataifa mawili 

Bwana Guterres pia amesisitiza kujitolea kwake, pamoja na kupitia kundi linaloundwa na Muungano wa Ulaya, Urusi, Marekani na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kushughulikia suala la Mashariki ya Kati, kusaidia Wapalestina na Waisraeli kusuluhisha mzozo huo kwa msingi wa maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya pande mbili. 

Kundi hilo, Jumamosi hii limetoa taarifa wakitoa wito kwa mamlaka za Israeli "kujizuia na kuepuka hatua ambazo zitaongeza hali kuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu." 

Kwa upande wa Wajumbe wa Kamati ya Waislamu, wamesema , "tuna wasiwasi juu ya taarifa za uchochezi za baadhi ya vikundi vya kisiasa, pamoja na rushaji wa roketi na kuanza tena urushaji wa maputo yanayowaka moto kutoka Gaza kuelekea Israeli, na mashambulio ya ardhi ya kilimo ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi. " 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNHCR, iliyotolewa hii leo asubuhi, watoto 29 wa Kipalestina, akiwemo mtoto mchanga wa kike, walijeruhiwa Mashariki mwa Jerusalem, pamoja na katika Jiji la Kale na kitongoji cha Sheikh Jarrah, na watoto wanane wa Palestina walikamatwa. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter