Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sinopharm ya China yaingizwa sokoni kukabili Covid-19

Chanjo dhidi ya COVID-19 ni msingi wa kukabili janga la corona
Unsplash/Ivan Diaz
Chanjo dhidi ya COVID-19 ni msingi wa kukabili janga la corona

Sinopharm ya China yaingizwa sokoni kukabili Covid-19

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO leo limeorodhesha chanjo ya Sinopharm kwa matumizi ya dharura dhidi ya COVID-19, na kuiruhusu isambazwe ulimwenguni.

Chanjo ya Sinopharm inayozalishwa na Beijing Bio-Institute of Biological Products Co Ltd, kampuni tanzu ya China National Biotec Group CNBG, zote za nchini China, inakuja baada ya chanjo nyingine kama Astrazeneca Oxford, Johnson & Johnson, Moderna, Pfizer-BioNTech kuwa tayari zimeizinishwa na kuingia kwenye matumizi. 

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa upatikanaji wa vifaa tiba wa WHO, Dkt  Mariângela Simão amesema, "kuongezwa kwa chanjo hii kuna uwezo wa kuharakisha upatikanaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazotafuta kulinda wafanyakazi wa afya na watu walio katika hatari. Tunamsihi mtengenezaji kushiriki katika mfumo wa COVAX na kuchangia lengo la usambazaji wa chanjo ulio na usawa." 

Utaratibu wa WHO Kuorodhesha Matumizi ya Dharura, EUL, ni sharti la usambazaji wa chanjo la COVAX. Pia unaruhusu nchi kuharakisha idhini yao ya kisheria ya kuagiza na kusimamia chanjo za COVID-19. 

EUL inatathmini ubora, usalama na ufanisi wa chanjo za COVID-19, pamoja na mipango ya usimamizi wa hatari na uendelevu wake. Tathmini hufanywa na kikundi cha tathmini ya bidhaa, kilichoundwa na wataalam wa sheria kutoka ulimwenguni kote na Kikundi cha Ushauri wa Kiufundi,TAG, inayohusika na kufanya tathmini ya faida ya hatari kwa pendekezo huru la ikiwa chanjo inaweza kuorodheshwa kwa matumizi ya dharura na ikiwa ni hivyo, chini ya masharti gani. 

Kwa uoande wa chanjo hii ya Sinopharm, tathmini ya WHO imejumuisha ukaguzi wa kituo cha uzalishaji. 

Chanjo ya Sinopharm ni chanjo inayotumia virusi visivyo hai ya SARS-CoV-2 (Vero Cell). Mahitaji yake rahisi ya uhifadhi yanaifanya ifae sana katika mazingira yenye rasilimali kidogo. Ni chanjo pia ya kwanza ambayo itakuwa na kipande cha karatasi ambacho hubadilika rangi  ikiwa chanjo itakabiliwa na joto  na hivyo kuwapa nafasi wahudumu wa afya kujua kama inaweza kutumika kwa usalama      au la.  

Bodi ya ushauri ya wataalamu wa kimataifa ya WHO, SAGE pia kimekamilisha ukaguzi wake wa chanjo. Kwa msingi wa ushahidi wote unaopatikana, WHO inapendekeza chanjo hii kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na zaidi, kwa utaratibu wa dozi mbili, ambapo dozi ya kwanza na ya pili zinaweza kutenganishwa kwa wiki tatu hadi nne. Ufanisi wa chanjo ya ugonjwa na dalili na hospitalini ilikadiriwa kuwa asilimia 79, makundi yote ya umri yakiwa yameunganishwa.  

Watu wazima (zaidi ya umri wa miaka 60) wachache walihusishwa katika majaribio haya, kwa hivyo ufanisi hauwezi kukadiriwa katika kundi hili la umri. Lakini, WHO haipendekezi ukomo wa umri wa juu kwa chanjo hii kwa sababu data ya awali na data ya kinga ya mwili zinayoonyesha kuwa chanjo hiyo kusaidia kuwakinga hata watu wazee.