UN yatoa dola milioni 65 kusaidia masuala ya kibinadamu Tigray Ethiopia 

6 Mei 2021

Umoja wa Mataifa leo umetoa dola za Marekani milioni 65 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kibinadamu nchini Ethiopia. 

Zaidi ya watu milioni 16 wanahitaji msaada wa kibinadamu kote Ethiopia, ikiwa ni pamoja na wastani wa watu wanaokadiriwa kuwa milioni 4.5 katika eneo la Tigray. 

Mkuu wa masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock alisema “Maisha na uwezo wa kuishi wa Waethiopia umesambaratishwa na ukame, na watoto wanaugua utapiamlo. Na miezi sita katika vita huko Tigray, raia wanaendelea kubeba mzigo. Wanawake na wasichana wanalengwa na unyanyasaji wa kijinsia na kingono, na mamilioni ya watu wanajitahidi kupata huduma muhimu na chakula, haswa katika maeneo ya vijijini ambayo yamekatwa kabisa na mawasiliano na misaada. Tunahitaji kuongeza hatua za msaada wa kibinadamu sasa. "  

 

Fursa ya kuwafikia wenye uhitaji bado ni mtihani 

 

Fursa ya kuwafikiwa wale wote wanaohitaji msaada katika  jimbo la Tigray bado ni changamoto kubwa kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibi masuala ya dharira na misaada ya kibinadamu OCHA. 

 

Hatahivyo shirika hilo limesema, “wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanashirikiana na mamlaka kuvishinda vizuizi hivyo na kuweza kupata fursa ya kuwafikia wale wanaohitaji msaada na na pia kufika katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa hayafikiki katika ukanda wa Kusini-Mashariki wa nchi hiyo.” 

 

OCHA imesema wiki iliyopita msafara wa misaada ya kibinadamu uliweza kufika Samre, ambapo ulitoa msaada wa dharura wa chakula na lishe na kuandaa kliniki ya afya katika hospitali ya Samre. Ripoti hizi za hivi karibuni zinaonyesha kuboreka kwa fursa za kuwafikia wenye uhitaji mkubwa na inasisitiza udharura wa ufadhili wa ziada kusaidia watu ambao hapo awali hawangeweza kufikiwa na misaada. 

  

“Jumla ya dola milioni 40 zitatengwa kwa operesheni ya misaada huko Tigray na fedha hizo zitafadhili makazi ya dharura, maji safi, huduma za afya, kazi ya kuzuia na kupambana na visa vya unyanyasaji wa kijinsia na kingono, na mawasiliano ya dharura kusaidia huduma za misaada ya kibinadamu.” 

 

Kwa mujibu wa OCHA fedha hizo zinakuja wakati hali ya usalama huko Tigray inabaki kuwa tete, wafanyikazi wa misaada hawawezi kufikia wale wote wanaohitaji msaada, na wagonjwa wa COVID-19 wameripotiwa miongvoni mwa watu waliotawanywa Mekelle. 

 

Sehemu zingine za Ethiopia pia zahitaji msaada 

  

OCHA inasema “Dola milioni 25 zilizobaki zitagharamia shughuli za kibinadamu katika maeneo mengine ya Ethiopia, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na ukame katika majimbo ya Somalia na Oromia. Pia zitasaidia matibabu ya watoto walio na utapiamlo mkali na ukarabati wa mifumo ya maji, kusambaza maji kwa jamii zilizoathiriwa na ukame, na kuwezesha mashirika ya kibinadamu kuweka mapema vifaa vya kuokoa maisha.” 

Juhudi za sasa za misaada ya kibinadamu kote Ethiopia, pamoja na jimboni Tigray, bado haitoshi kukidhi mahitaji ya watu wote walioathirika.  

Shirika hilo la misaada ya kibinadamu limesema “Fedha za ziada zinahitajika, pamoja na fursa za ufikiaji kwa usalama maeneo yasiyofikika kwa watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu, na kuhakikisha mashirika ya misaada na serikali ya Ethiopia wanaongeza kasi ya msaada unaohitajika.” 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter