Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulemavu sio kulemaa - Fahad na Ester wa Geita, Tanzania 

Matumizi ya nukta nundu.
UN Photo/Rick Bajornas)
Matumizi ya nukta nundu.

Ulemavu sio kulemaa - Fahad na Ester wa Geita, Tanzania 

Haki za binadamu

Watu wawili wenye changamoto ya uoni hafifu wanaoishi katika halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Tanzania, wameungana kuanzisha mradi wa kutengeneza vyungu vya kupandia maua, kupikia na majiko ya udongo ili kuepuka utegemezi katika jamii kama yanavyohamasisha malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu, SDGs.

Hapa ni katika mji wa Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.  Bwana Fahad Michael na Bi Ester Robert wakazi wa halmashauri ya mji wa Geita wanakabiliwa na tatizo la uoni hafifu tangu walipozaliwa lakini wameamua kushirika katika kutimiza malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu hasa lile la 8 ambalo linalenga kukuza shughuli za uzalishaji, ubunifu wa kazi, ujasiriamali, ubunifu na uvumbuzi, na kuhamasisha urasimishaji na ukuaji wa biashara ndogo ndogo, ndogo na za kati, pamoja na upatikanaji wa huduma za kifedha. 

Wawili hao wanatengeneza vyungu kwa kutumia hisia huku ujuzi wa kufinyanga vyungu wanadai kuupata kwa wakufunzi wajasiriamali waliokuwa wakifika katika maeneo yao. 

Bi Esther Robert anaeleza kwa nini wameamua kuanzisha mradi huo, "unakuta wenye ulemavu wengi ni ombaomba kwa sababu yale mazingira ya kujitegemea anakuwa hajazoeshwa. Ina maana tukishajiwezesha hivyo tutaweza sisi wenyewe kula na kuwasaidia watu wengine wenye ulemavu."

Licha ya juhudi hizo, Bwana Fahadi anaeleza changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao, "mtu akitusaidia hela kwa mfano ya kununua udongo, chakula, kodi au hata eneo la kufanyia kazi kama mtu kaguswa na sisi, ina maana hata Mungu atamwongezea zaidi."  

 Kutokana na changamoto hizo, Bi Esther anatoa wito kwa jamii, hususani kwa wale wana jamiiwanaoishi na watu wenye ulemavu, "halafu ninaishauri jamii, isione kuwa umezaa mtoto mwenye ulemavu kuwa ni mkosi. Mtoto mwenye ulemavu anaweza kama watoto wengine."