Skip to main content

Watu milioni 155 wanakabiliwa na njaa na kuhitaji msaada wa duniani:WFP/FAO/EU 

Mama akiandaa chakula kwa ajili ya binti yake kwa kutumia nafaka alizozipata kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la  mpango wa chakula, WFP, Maiduguri, Nigeria.
© WFP/Oluwaseun Oluwamuyiwa
Mama akiandaa chakula kwa ajili ya binti yake kwa kutumia nafaka alizozipata kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula, WFP, Maiduguri, Nigeria.

Watu milioni 155 wanakabiliwa na njaa na kuhitaji msaada wa duniani:WFP/FAO/EU 

Msaada wa Kibinadamu

Idadi kubwa na inayoongezeka ya watu wanakabiliwa na njaa kali na wanahitaji msaada wa kuokoa maisha, huku idadi kubwa ya watu wenye njaa kali katika nchi zilizokumbwa na madhila 2020 ilifikia kiwango cha juu zaidi katika miaka mitano, iliyopita imesema ripoti ya kila mwaka iliyozinduliwa leo kwa pamoja na muungano wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kushughulikia mgogoro wa chakula. 

Ripoti hiyo ya “Mtandao wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa Chakula” inaonesha kuwa watu wasiopungua milioni 155 walokabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula katika viwango vibaya zaidi vya daraja la 3 katika nchi na maeneo 55 kwa mwaka 2020.  

Mtandao huo wa kimataifa ukijumuisha shiorika la chakula na kilimo FAO, lile la mpango wa chakula duniani WFP na Muungano wa Ulaya EU umesema, “hii inawakilisha ongezeko la karibu watu milioni 20 kutoka mwaka uliopita, na ni uthibitisho kwamba hali mbaya ya ukosefu mkubwa wa chakula imekuwa ikiongezeka kwa kasi zaidi katika miaka mitano iliyopita.” 

 

COVID-19 imezidisha zahma 

 

Mwaka mmoja baada ya janga la corona au COVID-19 kuenea ulimwenguni kote, toleo la 2021 la ripoti ya kimataiofa juu ya mgogoro wa Chakula (GRFC) inathibitisha kuwa janga hilo na hatua zinazohusiana za kudhibiti kusambaa zaidi zimesababisha athari mbaya zaidi kwa changamoto ambazo tayari zilikuwepo za awali, haswa mizozo na mabadiliko ya tabianchi. 

 

Matokeo ya janga hilo ya changamoto za kiuchumi zimeongeza pengo la usawa na kuanika udhaifu wa muundo wa mifumo ya chakula ya ndani na ya kimataifa ikigonga zaidi mazingira dhaifu na makundi yasiyojiweza. 

Hali mbaya zaidi ya mgogoro wa chakula mwaka 2020, iliongozwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ikifuatiwa na Yemen, Afghanistan, Jamhuri ya Kiarabu ya Siria, Sudan, kaskazini mwa Nigeria, Ethiopia, Sudan Kusini, Zimbabwe na Haiti. 

“Kwa pamoja maeneo na nchi hizi 10 zilikuwa makazi ya zaidi ya watu milioni 103 kati ya watu milioni 155 waliokabiliwa na njaa kali mmwa 2020,” imesema ripoti hiyo 

 

Nchi za Afrika ndio waathirika wakubwa 

 

Nchi za Afrika zimesalia kuwa wathiriwa wa uhaba mkubwa wa chakula.  Kwa mujibu wa ripoti “Karibu watu milioni 98 waliokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka 2020 walikuwa katika bara la Afrika, ambayo ni 63% ya sehemu zote zinazokumbwa na uhaba wa chakula duniani” 

Ukosefu mkubwa wa chakula ni kiwango cha mwisho kilichokithiri zaidi wcha daraja la 3 la njaa (IPC /CH 3).  

Hii inamaanisha kwamba watu hawawezi kulisha familia zao na wanaweza kulazimishwa kuuza mali za kaya kwa pesa taslimu, au kutegemea msaada wa nje, kuweza kuishi. 

Mkurugenzi wa FAO wa masuala ya dharura na mnepo Dominique Burgeon amesema “Kwa kifupi matokeo makubwa ya ripoti hii ni kwamba mwaka 2020 ulikuwa mwaka wa giza sana kwa ubinadamu, kwa njia zaidi ya moja. Kwa kweli, mateso yaliyosababishwa na janga la COVID-19 yalikuwa kwenye runinga zetu  kila jioni. Lakini kile ambacho ripoti hii pia inatuambia ni kwamba pamoja na masaibu hayo ya kibinadamu, wanawake, watoto na wanaume milioni 155 walikuwa wakivumilia mwaka 2020 kile tunachokiita viwango vya juu kabisa vya ukosefu wa chakula. Hiyo inawakilisha ongezeko la karibu watu milioni 20 ikilinganishwa toleo la mwisho la ripoti hii ya kimataifa kuhusu mgogoro wa chakula.” 

 

Chachu kubwa ya hali hii 

 

Migogoro na mizozo kwa mwaka 2020 ndio zilikuwa chachu kubwa changamoto ya chakulakatika kiwango cha kimataifa ikifuatiwa na mdororo wa kiuchumi na hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi. 

Ripoti imeongeza kuwa “Karibu watu milioni 100 walikuwa katika ukosefu mkubwa wa uhakika wa chakula kwenye maeneo na nchi 23 ambazo mizozo na ukosefu wa usalama zilikuwa chachu kubwa ya hali hiyo ikiwa ni ongezeko kubwa la idadi ya watu ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo walikuwa watu milioni 77.” 

 

Mdororo wa kiuchumi  kiuchumi, inayohusiana sana na hatua za kudhibiti janga la COVID-19, ilikuwa chanzo cha pili muhimu kilichochangia zaidi ya watu milioni 40 katika kuwa katika ukosefu mkubwa wa chakula katika maeneo na nchi wilaya 17 nalo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo walikuwa watu milioni 24 katika nchi 8. 

 

Hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi  ilikuwa ni sababu ya tatu ya msingi wa ukosefu wa chakula duniani na zaidi ya watu milioni 15 waliathiriwa mwaka 2020 kutokana na sababu hiyo. 

Bwana Burgeon ameongeza kuwa, “ripoti hii inatuambia kuwa mzozo unabaki kuwa sababu namba moja ya njaa kali. Kwa kweli, watu milioni 99 walikuwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika maeneo na nchi 23 ambazo mizozo na ukosefu wa usalama vilikuwa chanzo cha kwanza. Mizozo ilifuatiwa na mshtuko wa kiuchumi, ambao katika maeneo mengi ulikuwa tayari ni sababu hata kabla ya janga la COVID-19 kuanza, lakini janga hilo limezidisha hali kuwa vibaya zaidi. Changamoto za mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa kama vile ukame na mafuriko, zilichukuwanafasi ya tatu muhimu ya sababu zilizochangia njaa kali mwaka 2020. " 

 

Waathirika wanahitaji msaada wa haraka 

 

Watu walio katika shida ya chakula wanahitaji misaada mbalimbali, kuanzia msaada wa kuokoa maisha hadi msaada wa kuweza kujikimu kimaisha. 

Burgeon anasema, "kuzuia njaa iliyoenea isishike kasi mwaka 2021, hatua za kibinadamu zinahitajika sasa kuokoa maisha na kwa kiwango kikubwa. FAO iko mashinani ikitoa msaada wa maisha unaohitajika sana ili wakazi wa vijijini waendelee kuzalisha na kupata chakula. Lakini tunahitaji rasilimali haraka. Na kwa nini hivyo? Kwa sababu tunajua kutokana na uzoefu kwamba hata katika mazingira magumu ya shida, inawezekana kusaidia watu kuzalisha chakula kinachowaweka hai. Tunajua kuwa haijalishi ni nini, bila kujali hali waliyo nayo, wakulima ni wakulima na watajaribu kuweka kilimo mbele, hata katika mazingira magumu zaidi. Lengo letu kwa hivyo ni kuwasaidia waweze kulima. Kuzuia janga la njaa kunaanza na kuzalisha chakula mahali ambapo inahitajika zaidi.” 

Burgeone ameongeza kuwa wadau wote wanahitaji kufanyakazi pamoja kuanzia serikali za kitaifa, mashirika ya kikanda, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali au NGOs, asasi za kiraia na sekta binafsi ili kubadili kabisa mifumo ya uzalishaji wa chakula ili iwe jumuishi zaidi, yenye mnepo na endelevu. 

Mtandao wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na njaa unataka kuwe na jukumu la pamoja na ahadi za kisiasa zikisaidiwa na rasilimali za kutosha ili kukabiliana na mzigo mkubwa wa changamoto za mabadiliko ya tabianchi na hasa kwa wale walio hatarini na wasiojiweza. 

Mtandao wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa chakula unafadhiliwa na EU, FAO na WFP na aulianzishwa mwaka 2016 kwa wadau mbalimbali wa masuala ya kibinadamu kushirikiana katika kuzuia, kujiandaa na kupambana na mgogoro wa chakula na kusaidia kutimiza lengo namba 2 la maendeleo endelevu ambalo ni kutokomeza njaa.