Nyumba binafsi Nepal zatumiwa kuwahudumia wakunga, kisa? COVID-19

5 Mei 2021

“Fuata takwimu, wekeza kwa wakunga,” ndiyo maudhui ya siku ya wakunga duniani hii leo, ikizingatia kuwa takwimu mpya zilizochapishwa katika Ripoti mpya ya hali ya wakunga duniani zinaonesha kuwa kupata idadi sahihi ya wakunga mwaka 2035 kutaokoa takribani maisha ya wanawake na watoto milioni 4.3 kila mwaka. 

Ripoti hiyo inasema “uwekezaji huo bora pia utaepusha asilimia 67 ya vifo vya wajawazito, asilimia 64 ya watoto wachanga na asilimia 65 ya watoto wanaozaliwa wafu.” 

Katika kufanikisha harakati za kuleta mtoto mchanga duniani, wakunga, mathalani nchini Nepal, wameweka maisha yao hatarini wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19

Wakati wa janga hili, wakunga wamechukua hatua za ziada, “wakati mwingine kufikia maeneo ambayo ni magumu kufikika, wakitembea nyumba kwa nyumba au kusafiri masafa marefu wakiwa na kliniki zinazohamahama. Wakati mwingine hawatoki nyumbani kabisa baada ya kugeuza vyumba kwenye nyumba zao kuwa kliniki za wazazi ili kupunguza msongamano katika vituo vya afya,” imesema UNFPA katika wavuti wake, 

Akipigia upatu hoja hiyo ya umuhimu wa uwekezaji kwa wakunga Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Dkt. Natalia Kanem katika ujumbe wake amesema, “uwekezaji mkubwa unapaswa kwa wakunga iwe kwa stadi zao au mahala pa kazi ili kuwawezesha kuwa na stadi bora na kutoa mchango mkubwa.” 

Dkt. Kanem amesema kuzalisha watoto siyo kazi pekee ya mkunga, “mkunga pia anatoa huduma za mama na mtoto kabla mama hajajifungua, anatoa huduma za uzazi wa mpango, huduma za uzazi wa mpango na afya ya uzazi kwa vijana, kwa kifupi, anasongesha ustawi wa kiafya wa jamii yake.” 

Mkuu huyo wa UNFPA amesema uwekezaji kwa wakunga utawezesha wapate mafunzo mazuri na kuweza kuwa na ujuzi wa kubadilishana hata wanapokuwa pahala pa kazi  

Akigusia wakunga ambao wamegeuza makazi yao kuwa vituo vya kutoa huduma za uzazi, Dkt Kanem amesema “kujitoa huko ni rasilimali ya kipekee na hufanyika huku mifumo mingi ya afya ikiwategemea bila kuwapatia msaada wa kiueledi ambao wanahitaji. Hii itapunguza matarajio yetu ya kutokuwa na vifo vya wazazi ifikapo mwaka 2030.” 

Dkt. Kanem amesema ushahidi sasa hivi upo na kinachotakiwa kufanyika kinatambuliwa. “Mifumo yote ya afya kila mahali lazima itambue na ichukue hatua, kwa sababu kuwekeza kwa wakunga wenye uwezo ni moja ya njia za uhakika zaidi za kulinda uhai na afya na ustawi wa kila mtu.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter