Je wajua jawabu la afya ya mama mjamzito na mwanae?

5 Mei 2021

“Fuata takwimu, wekeza kwa wakunga,” ndiyo maudhui ya siku ya wakunga duniani hii leo, ikizingatia kuwa takwimu mpya zilizochapishwa katika Ripoti mpya ya hali ya wakunga duniani zinaonesha kuwa kupata idadi sahihi ya wakunga mwaka 2035 kutaokoa takribani maisha ya wanawake na watoto milioni 4.3 kila mwaka. Ili kulifanikisha lengo hilo, tayari UNFPA Tanzania imekuwa ikifadhili mafunzo kwa wauguzi na wakunga ambayo yameanza kuonesha mafaniko.

Huyu ni mmoja wa akina mama waliojifungua, akiwa bado chini ya usimamizi wa wauguzi na wakunga wataalam katika hospitali moja hapa jijini Dar es Salaam Tanzania, “nimekuja kujifungua nimepokelewa vizuri na wauguzi na wakunga na wamenihudumia vizuri, mpaka sasa ninaendelea vizuri mimi na mwanangu.” 

Ama hakika huduma nzuri kutoka kwa mkunga inaleta tabasamu katika jamii na ndio maana mama huyu ana ujumbe kwa wengine, “kwa hiyo nilikuwa natoa ushauri kwa akina mama wengine ambao wako nyumbani na ni wajawazito waendelee kuhudhuria kiliniki na kipindi wanapokaribia kujifungua waje hospital watapokelewa vizuri na wakunga na watahudumiwa vizuri. Wakunga wanaokoa maisha.”  

Ripoti hiyo iliyotolewa leo inathibitisha hilo analolisema mama huyu kwani inasema “uwekezaji bora kwa wakunga pia utaepusha asilimia 67 ya vifo vya wajawazito, asilimia 64 ya watoto wachanga na asilimia 65 ya watoto wanaozaliwa wafu” na ndio maana shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA nchini Tanzania limekuwa likifadhili mafunzo kwa wauguzi na wakunga, na huyu ni mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, “mimi ninaitwa Agnes Ndunguru ni mkunga mtaalam na nina uzoefu wa miaka 7 katika taaluma hii ya ukunga na katika hiyo miaka 7 nimewasaidia wajawazito zaidi ya 6,000 pamoja na watoto wachanga zaidi ya 2,000. Ninafurahia kuwa mkunga kwa sababu ninaokoa maisha ya mama na mtoto na mimi ni mtu wa kwanza kumshika mtoto mchanga ambaye anatoka kwa mama yake. Na pia furaha yangu kubwa ni kusababisha furaha kwa watu wengine katika jamii, kwa sababu wakifurahi wao kwa kupata mtoto na mama mjamzito akitoka akiwa salama, basi na mimi ninafurahi.” 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter