Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata kukosesha maelfu ya watu Sudan Kusini huduma muhimu

Mama na mwanae wa umri wa miezi tisa wakilala chini ya neti iliyotolewa na UNICEF kwenye jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.
© UNICEF/Mark Naftalin
Mama na mwanae wa umri wa miezi tisa wakilala chini ya neti iliyotolewa na UNICEF kwenye jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.

Ukata kukosesha maelfu ya watu Sudan Kusini huduma muhimu

Afya

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, hii leo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Juba, Sudan Kusini, limeonya kuwa zaidi ya watu 800,000 nchini Sudan Kusini wanaotegemea IOM kupata huduma zao za afya wanaweza kukabiliwa na upungufu wa huduma za kuokoa maisha ifikapo mwezi Juni ikiwa wito wa haraka wa ufadhili wa kibinadamu hautatimizwa. 

Leo Mei, 04, IOM imetoa ombi la dharura la ufadhili ili kuweza kuendelea kutoa huduma, za gharama nafuu za afya kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi nchini Sudan Kusini. 

Shirika hilo limetngaza kuwa linahitaji dola za kimarekani 744,175 kwa mwezi ili kuendelea kutoa huduma ya kuokoa maisha. Hii ni sawa na dola 11 kwa kila mlegwa kwa mwaka, chini sana kuliko bei iliyoidhinishwa na ya Dola za Kimarekani 63.50 kwa kila mnufaika kwa mwaka. 

IOM inasema wakimbizi wa ndani, IDPs, watu waliorejea na walioathiriwa na mizozo ambao tayari wanaishi katika hali mbaya hivi karibuni wanaweza kukabiliwa na hatari kubwa zaidi kwa maisha yao na afya yao kutokana na janga la COVID-19 na mwanzo wa msimu wa mvua na mafuriko. 

“Wanawake na watoto, wazee na watu wanaoishi na ulemavu wako katika hatari ya kupoteza huduma za msingi za afya. Huduma hizi ni pamoja na afya ya mama na mtoto, pamoja na uchunguzi wa watoto chini ya miaka mitano kugundua utapiamlo; huduma za afya ya uzazi na upimaji na matibabu ya Virusi vya UKIMWI, VVU / UKIMWI na kifua kikuu.” Imeeleza taarifa ya IOM.  

"Katika mwaka uliopita, tumejifunza kwa ugumu kwamba wakati watu wengine hawana huduma za afya, kila mtu anaweza kuwa katika hatari. Afya sio anasa, ni haki na lazima. Lazima tuhamasishe ili kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.” Amesema Jacqueline Weekers, Mkurugenzi wa Afya ya Uhamiaji kwa IOM. 

IOM inaarifu kuwa kabla ya kuzuka kwa COVID-19, mfumo wa afya wa Sudan Kusini tayari ulikuwa umezidiwa na unategemea sana watendaji wa kibinadamu ambao sasa wanakabiliwa na upungufu wa ufadhili.