Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu zikiendelea Colombia, Umoja wa Mataifa wataka utulivu

Cali, jiji lililoko magharibi mwa Colombia.
UN News/Laura Quinones
Cali, jiji lililoko magharibi mwa Colombia.

Vurugu zikiendelea Colombia, Umoja wa Mataifa wataka utulivu

Amani na Usalama

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR leo imetoa tahadhari kubwa juu ya vurugu zilizotokea usiku wa kuamkia leo katika mji wa Cali nchini Colombia, ambapo watu kadhaa wameripotiwa kuuawa na kujeruhiwa wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanaji. 

Msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu Marta Hurtado akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao mjini Geneva Uswisi amesema kuwa ofisi ya OHCHR nchini Colombia inafanya kazi ili kudhibitisha idadi kamili ya majeruhi, na kubainisha jinsi tukio hilo lilivyotokea huko Cali. 

"Tumeshitushwa sana na matukio yanayoendelea huko na tunasisitiza mshikamano wetu na wale ambao wamepoteza maisha yao, pamoja na waliojeruhiwa na familia zao", 

Bwana Hurtado ameongeza kuwa watetezi wa haki za binadamu pia wameripoti kuwa walinyanyaswa na kutishiwa. 

Maandamano hayo, ambayo yalianza Jumatano iliyopita kupingha mageuzi ya ushuru uliopendekezwa, yaliendelea licha ya tangazo kutoka kwa Rais wa Colombia siku ya Jumapili kwamba muswada wa mageuzi utaondolewa kutoka bungeni. Waziri wa Fedha pia anaripotiwa kujiuzulu. 

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, maandamano mengi hadi sasa yamekuwa ya amani lakini ofisi hiyo imepokea madai ya vifo vya watu wasiopungua 14 katika maeneo tofauti nchini Colombia, pamoja na afisa wa polisi mmoja, tangu maandamano hayo yaanze. 

Hali ya wasiwasi yatanda 

Mse,maji huyo ameongeza kuwa kumekuwa pia na wito wa "maandamano makubwa" kesho Jumatano. 

"Kutokana na hali ya wasiwasi mkubwa , na kutokana na ukweli kwamba wanajeshi na maafisa wa polisi wamepelekwa kufuatilia maandamano hayo, tunatoa wito wa kuwa na utulivu", msemaji wa OHCHR amesema. 

Pia ameikumbusha mamlaka juu ya jukumu lao la kulinda haki za binadamu, pamoja na haki ya kuishi na usalama wa mtu, na kuwezesha utekelezaji wa haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani. 

“Tunasisitiza pia kwamba maafisa wa kutekeleza sheria wanapaswa kuzingatia kanuni za uhalali, tahadhari, ulazima na uwiano wakati wakisimamia  maandamano hayo. Silaha za moto zinaweza kutumiwa kama hatua ya mwisho dhidi ya tishio la maisha au la kuumizwa vibaya.”