Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya wakunga tutaongelea umuhimu wa kuwekeza kwa mkunga – Chama cha wakunga Tanzania 

Adrian Uhesi, Muuguzi Mkunga katika hospitali ya kumbukumbu ya Kairuki jijini Dar es salaam, nchini Tanzania.
UNIC Dar es salaam/Stella Vuzo
Adrian Uhesi, Muuguzi Mkunga katika hospitali ya kumbukumbu ya Kairuki jijini Dar es salaam, nchini Tanzania.

Siku ya wakunga tutaongelea umuhimu wa kuwekeza kwa mkunga – Chama cha wakunga Tanzania 

Afya

Kuelekea siku ya wakunga duniani hapo kesho, Chama cha wakunga nchini Tanzania, TAMA kupitia kwa ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA, limeeleza kuwa litaitumia siku hiyo kujadili umuhimu wa kuwekeza kwa mkunga.  

Feddy Mwanga ni Rais wa TAMA anasema, “tutanya shughuli nyingi za kimtandao na kwa kutumia vyombo vya habari tutafanya kongamano ambalo litakuwa na mahudhurio, na vilevile kwa njia ya mtandao, ambalo tutafanya pamoja na Chuo Kikuu kishiriki cha Muhimbili.” 

Kuhusu ni kwa nini mwaka huu wameamua kujadili suala la umuhimu wa kuwekeza kwa wakunga, Rais huyo wa Chama cha wakunga Tanzania, Bi. Mwanga anaeleza, “tutaongelea habar iza uwekezaji, umuhimu wa kuwekeza kwa mkunga, kwa sababu kaulimbiu yetu ya mwaka huu inasema fuata takwimu, wekeza kwa mkunga.” 

Na ni takwimu gani hizo zinazozungumziwa? Bi. Mwanga anafunguka, 

“zimefanyika tafiti, na katika ripoti ya UNFPA ya Desemba mwaka 2020 imeonesha kabisa kwamba mkunga aliyeelimishwa kwa kiwango cha kimataifa na ambaye anasimamiwa vizuri na akapewa mazingira wezeshi ya kufanyia kazi anaweza akatoa huduma ya kuokoa maisha ya mama na mtoto hadi asilimia 90. Na vilevile kuepusha vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 65 na pia kuzuia kuzaliwa kwa watoto wasio riziki (wanaofia tumboni), kwa asilimia 64. Hizi asilimia ni kubwa sana kwa mchango wa wakunga katika kuokoa maisha na kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi.”