Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yakaribisha tangazo la Sweden kutoa chanjo ya COVID-19 kwa ajili ya nchi za kipato duni 

Muhudumu wa afya akimchanja mtu wa pili kupata chanjo ya COVID-19 nchini Angola kwa mfumo wa COVAX.
© UNICEF/COVAX/Carlos César
Muhudumu wa afya akimchanja mtu wa pili kupata chanjo ya COVID-19 nchini Angola kwa mfumo wa COVAX.

WHO yakaribisha tangazo la Sweden kutoa chanjo ya COVID-19 kwa ajili ya nchi za kipato duni 

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amekaribisha tangazo la Serikali ya Sweden leo kuchangia dozi milioni 1 za chanjo ya AstraZeneca kwa mkakati wa kimataifa wa kuhakikisha kila nchi inapata chanjo unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, COVAX ili ziweze kuokoa maisha kwa watu walio katika hatari kutokana na COVID-19 katika nchi zenye kipato duni. 

Dkt Tedros, amenukuliwa alipokutana na Waziri wa ushirikiano wa maendeleo wa Sweden Bwana Per Olsson Fridh wakati za wa ziara ya kiongozi huyo wa Sweden katika makao makuu ya WHO mjini Geneva Uswisi hii leo akisema, "tangazo la Sweden kwamba watachangia dozi milioni 1 za chanjo za COVID-19 kwa COVAX ni ishara nzuri ambayo inapaswa kuigwa haraka, na mara kwa mara, na serikali nyingine ulimwenguni ili kuharakisha utoaji sawa wa chanjo ulimwenguni." 

COVAX inahitaji haraka dozi milioni 20 wakati wa robo ya pili ya mwaka 2021 ili kufidia muingiliano katika usambazaji uliosababishwa na mahitaji ya ziada ya chanjo nchini India ambako ndiko aliko msambazaji mkuu wa AstraZeneca. 

Dk Tedros ameongeza kwamba, "msaada kama huo utahakikisha kwamba watu katika nchi zilizo katika mazingira magumu, hasa, barani Afrika, wataweza kupokea dozi zao za pili kupitia mpango wa COVAX. Msaada wa ukarimu wa Sweden ni wa wakati muafaka kwani unakuja wakati ambapo ulimwengu unahitaji zaidi. " 

WHO na wadau wake wanahamasisha nchi nyingine kutoa michango, kama huu uliofanywa na Sweden kuchangia chanjo kutoka katika akiba zao ili kuongeza chanjo kwa COVAX iweze kuongeza wigo wa chanjo katika nchi zenye uchumi wa chini na kuhakikisha idadi ya watu katika maeneo kama hayo wanapata dozi za pili za chanjo zinazohitajika. Nchi nyingine kadhaa zimetoa ahadi kama hizo hivi karibuni, ikiwemo New Zealand na Ufaransa.