Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wenye ulemavu Burundi waamua kuutekeleza wito wa UN kwa vitendo 

Kuwa na ulemavu siyo ukomo wa maisha.
NICEF/Sebastian Rich
Kuwa na ulemavu siyo ukomo wa maisha.

Watu wenye ulemavu Burundi waamua kuutekeleza wito wa UN kwa vitendo 

Haki za binadamu

Nchini Burundi, Dany Kasembe, mwenye ulemavu wa mguu, ameamua kuwashirikisha wenzake katika kuutekeleza wito wa Umoja wa Mataifa kwa vitendo, wito ambao unataka uwepo wa dunia ambayo watu wote wana uwezo wa kupata fursa sawa na pia ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika jamii ikiwemo katika hatua za kukabiliana na kujikwamua na janga la corona au COVID-19. 

Mjini Rumonge mji ulioko kusini mwa magharibi mwa nchi ya Burundi. Kama kawaida, maisha yanaendeshwa ziwani Tanganyika nyakati za asubuhi ikiwa ni kipindi cha uvuvi na mchana katika nyanja mbalimbali za maisha utawakuta wazee kwa vijana wakijihusisha na biashara. 

Kama walivyoumbika binadamu kwa namna mbali mbali, ikaandikwa asiyefanya kazi na asile, baadhi ya watu wenye ulemavu mjini humo wamejibunia mbinu za kuendesha maisha kupitia sanaa. Dany Kasembe, ndiye kiongozi, amewakusanya watu wenye ulemavu kwa lengo la kusaidiana nao kujipatia mahitaji yao wao wenyewe. Bwana Kasembe anasema,“maeneo haya ni ofisi ya watu wenye ulemavu hususani vijana kwa sababu watu wenye ulemavu vijana wanakuwa wanaathirika sana kulingana na jinsi wanavyochukuliwa kwenye jamii. Sasa sisi ni watu wenye ulemavu, na mimi ni kiongozi wa wenye ulemavu kwa hivyo ninajitahidi kufundisha wale ambao wana ulemavu hata ambao sio wenye ulemavu. Vijana wa kike wapo ambao wanajifunza kwa mfano tukichukulia mfano wa yule pale (Rahma Gateka) naye pia ameshafikia kiwango kizuri na amefundishwa hapa hapa maendeleo yake ni mazuri zaidi. Fani yetu ya uchoraji na ufinyanzi wa udongo ina faida. Inaweza ikakidhi mahitaji yako na inaweza ikakutengenezea mahitaji mengine.” 

Kwa upande wa uchoraji, Rahma Gateka anakubaliana na kwamba watu wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu endapo wameshikamana bila ubaguzi, wanaweza kufikia maendeleo kwa pamoja, “nilikuwa sijui nitasalimia vipi na mtu ambaye ni kiziwi na hazungumzi, sisi tumezoea kuwaita mabubu. Ila kwa sasa hivi wako hapa, tunashida nao hapa tunasoma nao lugha ya ishara. Yaani sasa hivi bubu akija akanisalimia ninamjibu kwa lugha ya ishara kwa sababu tuna kama miezi miwili hivi tunafundishwa na mwalimu ambaye ni kiziwi ila anaongea kwa ishara zake. Hakuna fani isiyolipa ila ni uvumilivu. Sisi tumefunzwa hapa kuwa na uvumilivu. Tumefunzwa kuwa tusiharakie pesa isipokuwa tuharakie kuelewa fani kuiweka kichwani.”  

Uchoraji wao, huwa wanauelekeza katika vitu asili kwa nchi na kuchukuliwa kama Sanaa ya kitalii, anaeleza Ramha Gateka “vitu ambavyo nimeshavichora kwa mikono yangu ni vingi. Nilishachora wakaja wageni kutoka ng’ambo wakaja wakachukua. Kuna picha nilichora tunaziita ‘abstract painting’ maana yake ni picha ambazo unachora kwa mawazo yako. Nimemchora Mandera na kila mtu akija anaona ni yeye. Nimemchora Obama na pia Bob Marley ambaye alikuwa anawatetea wanyonge.” 

IRAMBONA Walda aliyehitimu ufundi cherehani, anasema kuwa hatapumzika mpaka pale nae atakapoanzisha  shirika japo kunaripotiwa uhaba wa vifaa na uzito katika kujifunza kwa kuwa mwalimu wake ni mtu mwenye ulemavu wa kuongea na ni kiziwi, “kabla ya kujifunza ufundi cherehani tulianza kufundishwa kuongea kwa kutumia vidole vya mikono. Baada ya kusoma tunapanga kuendeleza shirika la kujifunza.”  

Katika shirika ADH faida iliyomo haipimiki japokuwa pia changamoto hazikosi, hapa Dany Kasembe anataja kuwa janga la virusi vya Corona limekuja kuathiri zaidi maendeleo ya watu wenye ulemavu. 

 “kwa sababu ya jgonjwa hili la corona hatuna wageni. Unajua mgeni akiingia anaweza kukusaidia na kuinua kiwango lakini sasa hivi wageni hatuna, ni sisi wenyewe tunajiendeleza lakini hatuwezi tukaacha maana fani ni maisha yetu na tunajikita kwenye fani.” 

Bwana Kasembe anaomba jamii na serikali kutambua uwepo wa watu wenye ulemavu na wapewe fursa ya kupata elimu kama watu wengine, “jamii haitambui uelewa wa watu wenye ulemavu kiundani kwa hivyo tunaiomba serikali itusaidie kuwatafuta wenye ulemavu ususani mabubu ili wajue kuongea, wafahamu kusalimiana na watu, wajue kuwa wako na watu wengine.” 

Dany Kasembe ana miaka tisa akifundisha vijana wenye ulemavu wa viungo tofauti vya mwili na wasio na ulemavu mjini Rumonge, Burundi.