Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eneo la kusini mwa Madagascar hatarini kukumbwa na baa la njaa- WFP

Mama nchini Madagascar akisubiri mgao wa chakula huku akiwa amembeba mwanae katika taifa hilo linalokumbwa na ukame kwenye maeneo ya kusini.
© WFP/Fenoarisoa Ralaiharinony
Mama nchini Madagascar akisubiri mgao wa chakula huku akiwa amembeba mwanae katika taifa hilo linalokumbwa na ukame kwenye maeneo ya kusini.

Eneo la kusini mwa Madagascar hatarini kukumbwa na baa la njaa- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Hali ya ukame kupita kiasi huko kusini mwa Madagascar inazidi kutishia mamia ya maelfu ya wakazi wa eneo hilo kukumbwa na baa la njaa, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP katika taarifa yake iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo.

WFP imetaka hatua za dharura zichukuliwe ili kuepusha janga la kibinadamu linalonyemelea taifa hilo lililo katika bahari ya Hindi.

Shirika hilo linasema "wilaya nyingi za mikoa ya kusini iko katika hatari ya kuwa na dharura kwenye lishe ambapo kiwango kimataifa cha utapiamlo uliokithiri (GAM) miongoni mwa watoto wenye umri usiozidi miaka mitano kimeogezeka maradufu katika miezi minne iliyopita na kufikia asilimia 16.5 kwa mujibu wa takwimmu za sasa za Wizara ya Afya."

Maeneo yaliyoathirika zaidi

Wilaya zilizoathirika zaidi na ukame na hivyo kutishia baa la njaa ni Ambovombe ambako kiwango cha utapiamlo uliokithiri kimevuka asilimia 27, na hivyo kuweka maisha ya watoto hatarini. "Watoto wenye utapiamlo uliokithiri wako hatarini mara nne zaidi kufariki dunia kuliko watoto wenye afya.

Hali ya chakula katika eneo la Androy lililo kusini mwa Madagascar ni mbaya kiasi kwamba familia zinakusanya au kuokota chochote ambazo zinaona ili kulisha watoto wao.
© WFP/Fenoarisoa Ralaiharinony
Hali ya chakula katika eneo la Androy lililo kusini mwa Madagascar ni mbaya kiasi kwamba familia zinakusanya au kuokota chochote ambazo zinaona ili kulisha watoto wao.

Afisa mwandamizi wa operesheni za WFP nchini Madagascar Amer Daoudi amesema "kiwango cha janga ni kuliko unavyoweza kuamini. Iwapo hatutabadili mwelekeo wa janga hili, iwapo hatutawapatia chakula wakazi wa kusini mwa Magadagascar, familia zitakumbwa na njaa na watu watapoteza maisha."

Bwana Daoudi ametoa kauli hiyo leo baada ya kutembelea Sihanamaro, moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukame, na ziara hiyo alifanya akiwa ameambatana na mabalozi wanaowakilisha nchi zao Madagascar Pamoja na viongozi waandamizi wa serikali.

"Tumeshuhudia taswira za kuvunja moyo, taswira za watoto na familia zao wakiwa wanakabiliwa na njaa. Tunahitaji fedha zaidi na rasilimali zingine ili kusaidia wananchi wa Madagascar," amesema Bwana Daoudi.

Kiwango cha fedha kinachohitajika

WFP inasema itahitaji dola milioni 74 katika kipindi cha miezi 6 ijayo ili kuokoa maisha ya wakazi wa maeneo hayo ya kusini mwa Madagascar sambamba na kuzuia janga lisizidi kuenea.

Tangu kutangazwa kwa hali mbaya ya chakula huko Amboasary, WFP imekuwa ikisaidia watu 750,000 kwa kuwapatia chakula na fedha taslim kila mwezi.

Ukame wa mfululizo kusini mwa nchi hiyo umesababisha watu wapatao milioni 1.35 wawe na hitaji la dharura la chakula sambamba na huduma ya lishe.

Matarajio ya mavuno kwa mwaka huu wa 2021 ni madogo kwa kuwa kutokuwepo kwa mvua msimu wa upanzi ni kiashiria kuwa mavuno yatakuwa na hafifu na msim uwa mwambo wa kati ya Oktoba 2021 na Machi 2022 utakuwa mgumu zaidi.