Jamhuri ya Korea yatoa msaada wa mchele kwa wakimbizi Uganda wakati WFP ikiendelea kukabiliwa na ukata

29 Aprili 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP leo limekaribisha mchango wa tani 4,500 za mchele kutoka Jamhuri ya Korea za kuwasaidia kwa chakula wakimbizi 392,000 wa Sudan Kusini wanaohifadhiwa nchini Uganda. 

Mkurugenzi wa WFP nchini Ugandan El-Khidir Daloum amersema "Jamhuri ya Korea imekuwa mshirika mkuwa wa kujitolea nchini Uganda, ikitoa msaada unaohitajika kwa wakimbizi kwani tumetaka kuendeleza operesheni inayosaidia wakimbizi milioni 1.27 nchini Uganda ambao asilimia 82 kati yao ni wanawake na watoto,"  

Daloum ameongeza kuwa mchango huo mpya unakaribishwa haswa kwani utaziba pengo la mwezi mmoja hadi miwili ya misaada ya kibinadamu wakati ambapo WFP inakabiliwa na upungufu wa ufadhili wa dola milioni 86 kwa miezi sita ijayo kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi hao.  

Kwa mantiki hiyo WFP imesema haiwezi kuhakikisha kutopunguza pesa za msaada kwa wakimbizi au mgao wa chakula kwa mara ya tatu tangu Aprili 2020. 

Jamhuri ya Korea, ambayo sasa ni mfadhili wa nne mkubwa wa WFP kwa ajili ya wakimbizi nchini Uganda, inatoa maelfu ya tani za mchele kila mwaka tangu 2018.  

Hii imeiwezesha WFP kuwapa watu walio katika mazingira magumu wanaokimbia mizozo msaada wa kuokoa maisha ambao huimarisha ulaji wao wa chakula na lishe bora wakati wakijitahidi kuanza maisha yao katika nchi mpya. 

 WFP itasambaza mchango huu wa hivi karibuni katika makazi ya Adjumani, Imvepi, Kiryandongo, Palorinya na kambi ya Rhino ili kukidhi mahitaji muhimu ya nafaka ya wakimbizi kwa mwezi wa Agosti na sehemu ya mwezi wa Septemba. 

"Muundo wa Uganda wa kukirimu wakimbizi unathaminiwa kimataifa, na ndio sababu Jamhuri ya Korea itaendelea kusaidia wakimbizi nchini kupitia WFP na mashirika wadau ya Umoja wa Mataifa” alisema balozi Ha Byung-Kyoo wa Jamhuri ya Korea mjini Kampala. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula limesema kujitolea kwa wafadhili kusaidia wakimbizi nchini Uganda hakujawahi kuwa muhimu zaidi kwani upungufu wa fedha wa WFP unakuja wakati uhakika wa chakula miongoni mwa wakimbizi unapungua. 

Utafiti wa WFP uliofanyika mwezi Machi mwaka huu uligundua kuwa asilimia 43 ya kaya za wakimbizi zilikuwa na lishe duni, na zaidi ya nusu ya kaya zote ziliripoti kutumia mikakati hasi ya kuishi.  

“Hii ilitokana sana na upungufu wa chakula uliozidi kuwa mbaya na kupunguzwa kwa mgawo ambao ulimaanisha familia zililazimika kukopa chakula au kula chakula kidogo au ilibidi waamue ni nani anakula na nani asile.” Umeongeza utafiti huo. 

 WFP ililazimika kupunguza mgao wa chakula wa wakimbizi kwa asilimia 30 mnamo Aprili 2020, kisha kwa nyongeza ya asilimia 10 mnamo Februari 2021 kwa sababu ya kukata wa fedha tangu 2019.  

Uwezekano wa kupunguzwa zaidi kwa mgao unaleta hatari kubwa kwa uhakika wa chakula wa wakimbizi na njia za kukabiliana na changamoto hiyo, ambayo inadhoofisha sana matakwa ya Uganda ya kutaka wakimbizim waweze kujitegemea. 

Kwa sasa Uganda inahifadhi wakimbizi milioni 1.47, mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya wakimbizi iliyohifadhiwa na nchi moja.  

Karibu asilimia 90 ya wakimbizi  hao yaani milioni 1.27 wanaishi katika makazi 13 ya vijijini ambapo wanawasili wakiwa na mali kidogo au bila chochote. Hii inawaacha maelfu ya wakimbizi hao kutegemea sana msada wa WFP. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter