Bei ya vifaa vya mtu kujipima mwenyewe VVU yashuka- Unitaid 

28 Aprili 2021

Shirika la kimataifa la kufanikisha uwepo wa tiba nafuu duniani, Unitaid leo limetangaza ongezeko la upatikanaji katika soko na kushuka kwa bei kwa asilimia 50 kwa vifaa vinavyotumiwa na mtu binafsi kujipima iwapo ana Virusi Vya Ukimwi, VVU au la.

Unitaid ambalo linaratibiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, limesema hatua ya leo inafuatia makubaliano na kampuni binafsi ya Viatris kupitia kampuni mamaMylan, ambapo kuanzia sasa vikasha vya kujipima VVU vinavyotumia damu vitauzwa kwa chini ya dola 2 kila kimoja katika nchi 135 zinazokidhi vigezo. 

Msemaji wa Unitaid, Herve Verhoosel amesema, “kitendo cha mtu kupata vifaa vya kujichunguza mwenyewe VVU kimetambuliwa kuwa kigezo muhimu katika kufikia lengo la kimataifa la asilimia 90 ya watu kufahamu iwapo wameambukizwa VVU au la. Katika kipindi cha miaka 6 iliyopita ,kiwango hicho cha kutambua hali ya VVU kwa mtu kilikuwa kimeongezeka kutoka asilimia 45 hadi 81.” 

Unitaid inasema kifaa hicho Pamoja na kumwezesha mtu kubaini iwapo na virusi au la, pia ni njia ya kuanza matibabu na kupunguza mzigo wa VVU duniani. 

Halikadhalika, shirika hilo linasema kifaa hicho ni muhimu zaidi kwa nchi za kipato cha chini  na kati, ambako unyanyapaa umeshamiri na changamoto za huduma za afya zinaweza kuwa vikwazo zaidi. 

Kwa mujibu wa Bwana Verhoosel, kupanuka kwa soko la vifaa hivyo vya kupima VVU kutapatia nchi fursa zaidi ya kuchagua pindi inapokuja kuamua kuhusu vifaa vya kujipima VVU na kisha kujumuisha kwenye mifumo ya afya, na hatimaye kusaidia watu milioni 8 ambao wanakadiriwa kutofahamu hali yao ya VVU. 

Akitoa ushuhuda wa matumizi ya vifaa hivyo kwa Afrika Kusini, Dkt. Thato Chidarikire, Mkurugenzi katika wizara ya afya ya nchi hiyo amesema, “kipindi cha zaidi ya miaka miwili ya kutekeleza upimaji wa VVU Afrika Kusini, kimeshuhudia faida ya matumizi ya vifaa hivyo katika uchunguzi. Tumefikia wanaume, wanawake wenye umri wa kati ya miaka 19 hadi 24 na pia makundi muhimu. Habari za kupunguzwa kwa bei kwa vifaa vya mtu kuchunguza mwenyewe VVU kwa kutumia damu zimepokelewa vizuri Afrika Kusini kwa kuwa hivi sasa tunanunua vifaa hivyo kwa fedha zetu.” 

Uwekezaji wa Unitaid katika usambazaji wa vikasha hivyo tangu mwaka 2015 umewezesha kusambazwa kwa vikasha milioni 5, ambapo vikasha milioni 21 vinatarajiwa kuwa vimesambazwa kati yam waka 2020 hadi 2023. 

Zaidi ya hapo tayari nchi 85 zimejumuisha vikasha hivyo vya kujipima VVU katika sera zao za afya. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter