Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 29 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi ukanda wa Sahel 

Amarcia ni mmoja wa watu milioni 1.5 waliofurushwa Niger kwa sababu ya mzozo eneo la Sahel kati.
IOM/Monica Chiriac
Amarcia ni mmoja wa watu milioni 1.5 waliofurushwa Niger kwa sababu ya mzozo eneo la Sahel kati.

Watu milioni 29 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi ukanda wa Sahel 

Msaada wa Kibinadamu

Rekodi mpya ya juu inaonesha kuwa watu milioni 29 katika nchi sita yaani Burkina Faso, kaskazini mwa Cameroon, Chad, Mali, Niger na kaskazini mashariki mwa Nigeria - sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi, hii ikiwa ni watu milioni tano zaidi ya mwaka jana.

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya shughuli za kibinadamu katika ukanda wa Sahel, kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, yameelezea wasiwasi wao kuhusu kuzidi kwa kasi kwa mgogoro wa Sahel ambao umesababisha madhila makubwa kwa binadamu katika ukanda huo. 

Marie-Pierre Poirier, Mkurugenzi wa Kanda wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, anasema, “wakati mgogoro wa Sahel unapojitokeza, kizazi kizima cha watoto kiko hatarini. Pamoja na matukio ya usalama kuendelea kuongezeka, athari kwa watoto ni mbaya. Idadi ya mashambulio ya vurugu iliongezeka mara nane katika Sahel ya Kati na kuongezeka mara tatu katika bonde la Ziwa Chad. Vurugu na ukosefu wa usalama vinavuruga sana huduma za kimsingi za kijamii: karibu shule 5,000 zimefungwa au hazifanyi kazi, kuhatarisha maisha ya baadaye ya mamia ya maelfu ya watoto, na watoto milioni 1.6 wanakadiriwa kuugua utapiamlo mkali. Ili kushughulikia mahitaji ya sasa ya idadi ya watu wakati tunajenga msingi wa maendeleo endelevu, tunahitaji mabadiliko ya dhana na kutenda pamoja na serikali na watu wa Sahel.” 

Naye Xavier Creach, Mratibu wa UNHCR Sahel na ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Afrika Magharibi na Kati anasema, “Jibu letu juu la shida isiyo ya kawaida ya kibinadamu na ulinzi, inayosababisha kuhama kwa mamilioni ya watu, lazima pia ijumuishe jamii zinazowakaribisha ambao kwa ukarimu hugawana rasilimali kidogo walizonazo. Lazima tuhakikishe kwamba jamii hizi zinaendelea kuishi kwa amani, wakati ambapo janga hili limekuwa na athari mbaya kwa maisha, hasa wale wanaoishi kwa kipato cha kila siku.” 

Fatoumata Haidara, Mkurugenzi wa Kanda wa Plan International kanda ya Sahel anasema wanawake na watoto ni miongoni mwa walio katika mazingira ya hatari zaidi  huku Mkurugenzi wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP katika kanda hiyo Chris Nikoi akisema kwamba ongezeko la bei ya vyakula nalo linasukumbuma mbali zaidi mlo wa msingi kwa mamilioni ya familia masiki ambao wanahangaika. “Tunahitaji msaada wa haraka kusaidia wale walioko katika uhitaji mkubwa na suluhisho la muda mrefu visababishi vikuu vya njaa na utapiamlo huko Sahel.” Anasisitiza Bwana Nikoi.  

Kwa upande wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibi misaada ya dharura, OCHA, Mkrugenzi wa kanda hiyo ya Sahel, Julie Belanger anasema, "hali hii isiyo na mfano inahitaji hatua za haraka, lakini kati ya changamoto kuu za kutoa misaada inayofaa inabaki upungufu wa fedha. Ni muhimu kutanguliza hatua za kibinadamu. Nyuma ya idadi na data, kuna hadithi za mateso ya wanadamu. Bila rasilimali za kutosha, mgogoro huo utazidi kuongezeka, kumomonyoa uimara wa jamii na kuweka mamilioni ya watoto, wanawake na wanaume katika hatari. Hadi kufikia sasa mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili, ni asilimia 9 tu ya dola bilioni 3.7 zinazohitajika zimepokelewa. Hii haitoshi.”