Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ana matumaini na mazungumzo ya kumaliza uhasama Cyprus

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Cyprus (UNFICYP) unadhibiti eneo maalum kati ya pande kinzani nchini Cyprus.
UN/Eskinder Debebe
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Cyprus (UNFICYP) unadhibiti eneo maalum kati ya pande kinzani nchini Cyprus.

Guterres ana matumaini na mazungumzo ya kumaliza uhasama Cyprus

Amani na Usalama

Hatua mpya ya Umoja wa Mataifa kusaka kumaliza wa miongo kadhaa nchini Cyprus kati ya raia wenye asili ya Ugiriki na wale wenye asili ya Uturuki, imeanza upya hii leo huko Geneva, Uswisi huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa na matumiani kuhusu fursa za kusongesha mpango huo.

Stephane Dujarric, ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu, amewaeleza waandishi wa Habari mjini Geneva, kuwa "Katibu Mkuu ameamua kuandaa mkutano huo kufuatia mashauriano yaliyofanyika miezi kadhaa kwa niaba yake na msaidizi wake Jane Holl Lute." Bi. Holl Lute amekuwa akifanya mashauriano hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu.

"Kama ambavyo tumekuwa tukisema mara kadhaa, lengo la mkutano huu litakuwa kubaini iwapo kuna msingi wa pamoja kwa pande kinzani kufanya mashauriano ili kupata suluhu ya kudumu ya suala la Cyprus katika muktadha unaoonekana."

Hali ya sasa imekuja miaka minne baada ya viongozi wa wagiriki wenye asili ya Cyprus na wagiriki wenye asili ya Uturuki kukutana nchini Uswisi kujadili mustakabali wa kisiwa hicho kilichoko bahari ya Mediteranea ambacho kina mgawanyiko mkubwa.

Mkutano wa sasa unaofanyika katika mji wa Crans Montana katika milima ya Alpine ulikwama baada ya wiki ya majadiliano juu ya masuala sita ikiwemo hakikisho la usalama, mipaka mipya ya kimaeneo na kushirikiana kwenye madaraka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akikutana na Ersin Tatar (kushoto) ambaye ni kiongozi wa wacyprus wenye asili ya Uturuki. Ni wakati wa mazungumzo yasiyo rasmi yanayoendelea Uswisi.
UN /Jean-Marc Ferré
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akikutana na Ersin Tatar (kushoto) ambaye ni kiongozi wa wacyprus wenye asili ya Uturuki. Ni wakati wa mazungumzo yasiyo rasmi yanayoendelea Uswisi.

Katika awamu ya sasa, Katibu Mkuu Guterres amepanga kuwa na mikutano ya siku tatu isiyo rasmi kuanzia leo mchana.

Mkutano wa kwanza wa pande mbili ulipangwa kuwa kati ya kiongozi wa wacyprus wenye asili ya Uturuki Ersin Tatar ukifuatiwa na mkutano na kiongozi wa waCyprus wenye asili ya Ugiriki Nicos Anastasiades.

Wakati Bwana Anastasiades tayari ameshiriki mashauriano yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa kuhusu mustakabali wa kisiwa hicho kwa amani, Bwana Tahar anaongoza ujumbe wa wacyprus wenye asili ya Uturuki ikiwa ni mara ya kwanza tangu awe rais mwezi Oktoba 2020.

"Katibu Mkuu kwa sasa ana uhakika," amesema Bwana Dujarric, "hili ni suala ambalo anafahamu vizuri, ameshashiriki tena kwenye majadiliano ya aina hii."

Mkutano wa sasa nchini Uswisi unajumuisha pia wajumbe kutoka Ugiriki, Uturuki na Uingereza, wote wakiwa wafadhili wa Cyprus ambao walikubaliana na uhuru wa kisiwa hicho mwaka 1960 na ambao kihistoria wamekuwa wakishikiri katika majadiliano.

Kufuatia kuanzishwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Cyprus (UNFICYP) mwaka 1964, Sweden ilipeleka kikosi  kwenye kisiwa hicho kilichoko kwenye bahari ya Mediterranea.  UN Photo
UN
Kufuatia kuanzishwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Cyprus (UNFICYP) mwaka 1964, Sweden ilipeleka kikosi kwenye kisiwa hicho kilichoko kwenye bahari ya Mediterranea. UN Photo

Maandamano ya Amani

Mkutano wa sasa umefanyika baada ya wacyprus wa asili ya Uturuki na wale wenye asili ya Ugiriki kuandamana kwa amani mwishoni wa wiki huko Nicosia, moja ya miji mikuu barani Ulaya ambao umekuwa na mgawanyiko kwa zaidi ya miongo minne sasa.

"Katibu Mkuu atasongesha masuala kulingana na matokeo ya mazungumzo haya yasiyo rasmi," amesema Dujarric akiongeza "kama tulivyosema, na kama nilivyosema nadhani mwezi Februari na mara nyingine nyingi jijini New York- pande husika zinakaribishwa kuwa bunifu na Katibu Mkuu atazihamasisha ziendelee, unajua kutumia lugha ya kidiplomasia kwa uwazi na kwa uaminifu. Kwa mara nyingine tena ni muhimu kusisitiza kuwa haya ni mazungumzo yasiyo rasmi."

Kikosi cha UN tangu mwaka 1964

Katika kusaidia kuweka usalama kwenye kisiwa hicho, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, UNFICYP nchini Cyprus tangu mwaka 1964. Lengo ni kuepusha mapigano kati ya wacyprus wenye asili ya Ugiriki na wale wenye asili ya Uturuki.

Kamanda wa sasa wa kikosi hicho ni Meja Jenerali Ingrid Gjerde kutoka Norway.

Majukumu ya ujumbe huo yaliongezeka mwaka 1974 kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na kikundi kinachotaka muungano na Ugiriki, na kisha Uturuki iliingilia kijeshi na jeshi lake kukamata eneo la kaskazini la kisiwa hicho.

TAGS: Cyprus, Ugiriki, Uturuki, UNFICYP