Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko ya karibuni Moghadishu yananitia hofu:Guterres 

Mojawapo ya picha kutoka maktaba ikionesha shambulio la kigaidi kwenye hoteli ya Benadir huko Mogadishu Somalia tarehe 25 Agosti mwaka 2016.
UN Somalia
Mojawapo ya picha kutoka maktaba ikionesha shambulio la kigaidi kwenye hoteli ya Benadir huko Mogadishu Somalia tarehe 25 Agosti mwaka 2016.

Machafuko ya karibuni Moghadishu yananitia hofu:Guterres 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anatiwa wasiwasi mkubwa na machafuko yaliyozuka karibuni mjini Moghadishu Somalia. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Jumatatu jioni Guterres amesema machafuko hayo ya silaha yanahatarisha zaidi hali ya usalama na amerejelea wito wake kwa wadau wote nchini Somalia kujizuia na machafuko zaidi na kuwataka kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo na maafikiano. 

Jumatatu jioni milio ya risasi ilisikika baada ya watu kumiminika mitaani mjini Moghadishu wakipinga kuongezwa muda wa utawala wa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wakitaka uchaguzi ufanyike. 

Hatua hiyo pia imesababisha kuzuka kwa machafuko baina ya pande hasimu kwenye vikosi vya usalama. 

Katibu Mkuu Guterres amezitaka pande za wadau wote nchi Somalia kuanza tena mazungumzo mara moja na kufikia makubaliano kwa kuzingatia muundo wa uchaguzi wa 17 Septemba mwaka jana na mapendekezo ya Baidoa.