Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yasaidiana na serikali CAR kupunguza athari za kimazingira

Ukarabati wa dampo la Kolongo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. kwa msaada wa MINUSCA
MINUSCA / Erick-Christian AHOUNOU
Ukarabati wa dampo la Kolongo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. kwa msaada wa MINUSCA

MINUSCA yasaidiana na serikali CAR kupunguza athari za kimazingira

Amani na Usalama

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR ujulikanao kama MINUSCA, umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kupunguza athari za kimazingira kwa raia wa nchi hiyo hususan katika udongo, hewa na katika vyanzo vya maji .

Katika dampo kubwa la taka la Kolongo lililopo kilometa takriban 7 kutoka mji mkuu wa CAR Bangui nchini CAR wahandisi wa kikosi cha Indonesia kwenye mpango wa MINUSCA wako katika harakati za ukusanyaji na uhifadhi wa taka wakishirikiana na wahudumu wengine wa manispaa wanaohusika na udhibiti wa taka. 

Mradi huu wa ukusanyaji na uhifadhi wa taka ni moja ya miradi ambayo inatekelezwa na MINUSCA kama sehemu ya juhudi na sera zake za kupunguza athari za mazingira nchini humo,  mbali na jukumu kubwa la ulinzi wa amani walilonalo. 

Lizbeth Cullity, ni naibu mwakilishi maalum wa MINUSCA nchini humo,“Sote tunahitaji dunia bora na yenye afya ili kutuhakikishia uhai wetu, hii inamaanisha kwamba ni afya yetu na furaha yetu.” 

Kazi kubwa katika mradi huu ni kuhakikisha dampo hilo la manispaa limekuwa tambarare na taka zinahifadhiwa vyema. 

Tayari kuna mashimo makubwa matatu ya kutupa taka hizo kwenye eneo hili na MINUSCA inachimba na kujenga mengine matatu kupitia ofisi ya Umoja wa Mataifa ya huduma za miradi UNOPS ambaye ni mdau mkubwa wa miradi ya Umoja wa Mataifa. 

Kudhibiti taka ngumu ni mtihani nchini CAR, Waziri wa mazingira na maendeleo endelevu wa nchi hiyo ni Thierry Kamach anathibitisha “Kwa hakika udhibiti wa taka ngumu kwa manispaa ni changamoto kubwa , mbali ya kukusanya taka kuzidhibiti na mchakato wa kuzichakachua unaleta matatizo makubwa bila kujali ni kiwango gani cha taka  kinachohitaki kuchakachuliwa.” 

MINUSCA inasema mradi huu utaboresha udhibiti wa taka ngumu kwa manispaa ya Bangui na kupunguza athari za taka hizo kwa wakazi wa Kolongo na mji mkuu Banguai na utagharimu jumla ya dola milioni 2.83.